Habari

Daktari alaumu uchawi Kilifi kwa umaskini wake

November 9th, 2019 2 min read

Na MAUREEN ONGALA

DAKTARI wa mifugo aliyestaafu katika Kaunti ya Kilifi, anadai kuwa uchawi umemsababishia umaskini mkubwa maishani mwake.

Mzee Shida Mramba kutoka kijiji cha Fumbini-Searhose, eneobunge la Kilifi Kaskazini, anasema alipoteza mali yake yote kutokana na watu wa eneo hilo kumwendea mbio kutumia urogi na mitishamba.

Bw Mramba, 62, aliambia Taifa Jumapili akiwa katika nyumba yake ya matope kwamba, alipokuwa akifanya kazi, alijikusanyia mali ya kutosha na akaanzisha miradi mingi ili kukimu mahitaji ya wake zake watatu na zaidi ya watoto kumi.

“Kinu cha kusaga nafaka kupata unga nilichonunua miaka saba iliyopita kiliharibika siku chache baada ya kuanza kazi. Na mradi wa kuku pia ulisambaratika baada ya kuku hao kuvamiwa na funza. Isitoshe, ng’ombe wa maziwa nilionunua nao walikufa.

Alieleza kuwa alianzisha miradi hiyo kama njia ya kuzalisha mapato ya ziada kwa familia yake alipokuwa akifanya kazi kama daktari wa mifugo.

Kinu alikinunua baada ya kuchukua mkopo wa Sh60,000 ili kuwafaa wanawake ambao walikuwa wakitembea mwendo mrefu kusaga nafaka zao mjini Kilifi.

“Kinu kilikumbwa na hitilafu baada ya muda mfupi. Kilianza kutetemeka na kurusha mahindi nje. Nilimwita mekanika lakini badala ya kukikarabati alichukua kipuri kimoja na kutoweka. Hadi sasa sijaweza kumwona wala kumfikia hata kwa simu,” akaeleza kwa masikitiko.

Maendeleo yasambaratika

Mzee wa kijiji hicho, Bw Daniel Wanje alisema vitendo vya uchawi vimesambaratisha maendeleo na masomo katika eneo hilo, hali ambayo imetumbikiza wengi wao katika lindi la umasikini.

“Hapo zamani, wanakijiji walikuwa wakiwatambua washukiwa wa uchawi kwa usaidizi ya watu wenye uwezo maalum wa kufanya hivyo. Baada ya kutambuliwa, wangelishwa kiapo na kutakaswa kisha kuonywa wasirudie kitendo hicho wasije wakafa. Hii ilisaidia kupunguza visa vya uchawi,” akasema Mzee Wanje.

Lakini punde tu serikali ilipopiga marufuku kutambuliwa kwa washukiwa wa uchawi kwa hofu ya wao kuuawa, anasema mambo yalianza kubadilika.

“Tunaficha shida kubwa huku jamii yetu ikiendelea kurudi nyuma kimaendeleo na hata kuangamizwa kabisa,” akaongeza Wanje.