Habari

Daktari aliyempasua mwanamke titi akafariki sasa aililia mahakama

October 25th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MTAALAMU wa tiba za ngozi aliyemfanyia mwanamke upasuaji wa kufanya titi lake linenepe na hatimaye kusababisha kifo chake sasa anaiomba mahakama kuu ishurutishe Nairobi Hospital imrejeshe kazini.

Hospitali hiyo ilimwachisha kazi  Profesa Stanley Ominde Khainga baada ya kufariki kwa Bi June Mulupi mnamo Juni 5, 2018.

Prof Khainga anasema katika kesi aliyowasilisha katika mahakama ya kuamua mizozo baina ya wafanyakazi na waajiri (ELRC) haki zake zilikandamizwa na Nairobi Hospital iliyositisha huduma zake.

Prof Khainga anasema katika kesi iliyoshtakiwa na wakili Profesa Kiama Wangai kwamba uchunguzi haukufanywa kubaini kilichosababisha kifo cha mwanamke huyo.

Anasema kuwa utaratibu wa kumfanyia upasuaji  uliochukua muda wa saa nne ulifuatwa na hatimaye akaruhusiwa kuondoka hospitalini.

Mlalamishi anasema hakumfanyia upasuaji June akiwa peke yake bali alikuwa na wasaidizi wengine waliokuwa wanatoa ushauri.

Prof Khainga anasema kuwa marehemu alifanyiwa upasuaji wa kwanza mnamo Machi 24, 2018 na ukafaulu.

Alikuwa arudi tena kufanyiwa upasuaji tena ndipo titi lake la kushoto lisawazishwe na lile la kulia.

“Titi la upande wa kushoto wa mwendazake lilikuwa ndogo kuliko lile la upande wa kulia. Lilipasa lisawazishwe na la kulia ,” asema Prof Khainga katika ushahidi aliowasilisha mahakamani.

Prof Khainga anasema kuwa Bw Joseph Mulupi,  mumewe June alimtembelea hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji na kuzungumza naye.

Hatimaye mgonjwa huyo aliathirika na upasuaji huo na kuaga dunia. Hospitali ilimsimamisha kazi na kumzuia kuwalaza wagonjwa mle.

Anasema haki zake za kikatiba zilikandamizwa na anaomba korti iamuru akubaliwe kuendelea kuhudumu.

Kesi iliorodheshwa na Jaji Brian Oganyo kusikizwa Oktoba 31, 2018.

Mahakama ilimwamuru wakili Prof Wangai aikabidhi nakala za kesi hiyo hospitali hiyo ndipo iwasilishe majibu.