Kimataifa

Daktari amnyonga mpenzi kitandani hadi kufa kisha kupika mwili wake

April 23rd, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

DAKTARI kutoka Urusi amekiri kuwa alimuua, akamharibu sura kisha kupika baadhi ya sehemu za mwili wa mwanamke aliyekuwa mpenzi wake, baada ya kubaini kuwa alikuwa mwanamume mbeleni lakini akafanyiwa upasuaji wa kujibadili kuwa mwanamke.

Mikhail Tikhonov (pichani juu) mwenye umri wa miaka 27 aliambia polisi kuwa alipika baadhi ya viungo vya mwili wa mpenzi wake jikoni, kisha vilivyosalia akavitupa chooni.

Mikhail, ambaye ni daktari alikuwa ameenda kujiburudisha na mpenziwe Nina Surgutskaya, 25, katika eneo la Kursk usiku, kisha wakarejea nyumbani kwa Nina.

Wawili hao walikuwa wakifanya ngono wakati Mikhail alibaini kuwa mpenzi wake aliwahi kuwa mwanamume, lakini baadaye akatibiwa kwa upasuaji kuwa mwanamke.

Mara moja, alimnyonga wakiwa kitandani, kisha ili kuficha mauaji hayo, akaharibu sura ya maiti yake, mshukiwa alieleza wachunguzi.

Mikhail alizuiliwa kwa mahojiano wakati Nina alitoweka na mamake akapigia polisi ili wachunguze.

Ripoti ya polisi kuhusu kisa hicho ilisema Nina ndiye alikuwa amemwalika Mikhail nyumbani kwake (Nina), kisha wakaanza kunywa pombe na kufanya ngono, lakini Mikhail akagundua kuwa mpenzi wake alikuwa mwanamume mbeleni.

“Nina alijaribu kuendelea na ngono lakini wakati huo Mikhail akamnyanyua kwa kumshika shingoni na kumnyonga. Alimwachilia tu wakati aliona kuwa amekata roho,” afisa wa polisi akasema.

Baadaye, Mikhail aliamua kuutupa mwili, ambapo aliipeleka maiti hadi kwenye bafu, akakata sehemu za ndani na kuzikatakata kuwa vipande vidogo ambavyo alivitupa chooni.

Nyama ya maiti hiyo aliipika kwenye ‘Oven’ hadi ikayeyuka, kisha akaitupa chooni. Mwanamume huyo alipinga kuwa yeye ni mla watu, akisema alitupa nyama aliyopika chooni.

Kichwa na miguu aliviweka ndani ya mkoba, kisha akaenda navyo hadi nyumbani kwake, ripoti ya polisi ikasema. Baadaye alivitupa katika majaa ya takataka.

“Hakupata wakati wa kutupa kichwa na sehemu ya nyuma ya mgongo kwa kuwa alipatikana kabla afanye hivyo,” ripoti ya polisi ikasema.

Sasa daktari huyo anakumbana na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani ikiwa atapatikana na makosa hayo ya mauaji na kuharibu mwili.