Habari Mseto

Daktari ampasua mfungwa makalio na kumtoa simu!

December 1st, 2018 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

MFUNGWA mmoja wa gereza la Manyani, anauguza majeraha mwilini baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Moi, ili kutoa simu ambayo alikuwa ameificha katika sehemu ya makalio.

Mfungwa huyo anadaiwa kuwa alikuwa ameificha simu sehemu hiyo ili isionekane na maafisa wa kulinda gereza hilo.

Hata hivyo, alipoenda kuitoa, simu ilikataa kutoka na baadaye ikamfanya kuumwa na tumbo sana na kushindwa kwenda haja kubwa kwa siku tatu, mwishowe akifunguka kwa maafisa kuhusu kiini cha matatizo yake.

Maafisa hao walimkimbiza katika hospitali hiyo ambapo alipopigwa picha za X-ray, ilibainika kuwa simu ilikuwa imeingia mwilini baada ya kujisukuma ndani.

Madaktari katika kituo hicho cha afya walipendekeza kuwa mfungwa huyo afanyiwe upasuaji ili kuitoa simu yenyewe, mkuu wa hospitali Kagona Gitau akisema kuwa bado anaendelea kupata nafuu.

“Tutampa ruhusa kuondoka hivi karibuni lakini tutakua tukifuatilia hali yake katika kliniki ya wagonjwa wasio wa kulazwa,” akasema.

Mkuu wa gereza la Manyani Nicholas Maswai alisema kuwa wafungwa huwa wanaficha vitu visivyoruhusiwa kuwa gerezani namna hiyo ili visipatikane.