Habari za Kitaifa

Daktari apendekeza sadaka na fungu la kumi kutozwa ushuru

January 24th, 2024 2 min read

NA ERIC MATARA

HUENDA makanisa nchini yakaanza kutozwa ushuru wa mapato kwa pesa yanayokusanya kama sadaka na fungu la kumi iwapo Mahakama Kuu itakubaliana na daktari mmoja wa Nakuru anayedai kutoyatoza ushuru ni kukiuka Katiba.

Dkt Magare Gikenyi amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Nairobi akipinga vifungu vya Sheria ya Ushuru wa Mapato vinavyoruhusu makanisa kutolipia ushuru pesa za sadaka na fungu la kumi.

Katika kesi yake, Dkt Gikenyi anasema kwamba, sehemu 3(2) ya Sheria ya Mapato inakinzana na Katiba inayosema kila Mkenya anapaswa kulipa ushuru bila kujali sekta anayohudumu.

Haswa, analenga sehemu 13 ya Sheria ya Mapato ambayo inasamehe baadhi ya watu na mashirika, yakiwemo makanisa, kutolipa ushuru wa mapato.

Katika stakabadhi za kesi yake, anasema kwamba, fungu la kumi, sadaka na michango zinapaswa kutozwa ushuru ili kutimiza hitaji la Katiba la kutobagua yeyote katika ulipaji wa ushuru.

Anataka mahakama iamue na kutangaza kuwa sehemu 3(2) ya Sheria ya Mapato inabagua na hivyo, ni kinyume cha Katiba na haifai kuwepo.

Katika kesi yake, Daktari huyo anasema anataka makanisa yaorodheshwe katika mashirika yanayolipa ushuru akisema kulingana na ibara ya 201(b) ya Katiba, ni sharti kila Mkenya alipe ushuru.

Dkt Gikenyi analenga sehemu ya 13 ya sheria ya mapato anayosema inabagua na inakinzana na Katiba kwa sababu inaruhusu baadhi ya makundi ya watu na mashirika kutolipa ushuru

“Fungu la kumi, sadaka na matoleo mengine na watu wengine na mashirika yanayoruhusiwa kutolipa ushuru, wanapaswa kulipa kwa kuwa ibara ya 201 ya Katiba inasema hakuna anayefaa kubaguliwa,” anasema Dkt Gikenyi katika stakabadhi za kesi.

Anaomba mahakama itangaze kuwa, sehemu ya 3(2) ya sheria ya mapato inabagua, inakiuka katiba na haifai kuwepo kwa sababu inaruhusu baadhi ya watu kutolipa ushuru huku wengine wakilipa.

Anasema ubaguzi katika ulipaji ushuru unaongezea mzigo wanaolipa nchini Kenya.

Katika Kenya, fungu la kumi, sadaka na michango haichukuliwi kama mapato na faida au ajira na hazitambuliwi na sheria ya mapato.

Katika kesi yake, Dkt Gikenyi, anasema kwamba watu matajiri, makundi ya kutoa misaada, makanisa, misikiti, mahekalu na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yananufaika pakubwa kwa kuwa hayalipi ushuru ilhali yanaweza kusaidia kwa kulipa ushuru wa mapato.

Dkt Gikenyi anataka mahakama itoe agizo kuzuia serikali kutekeleza sheria yoyote anayodai, inaruhusu mtu au shirika kutolipa ushuru wa mapato.

Ametaja Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya, Seneti na Bunge la Kitaifa kama washtakiwa katika kesi hiyo ambayo amehusisha Baraza la Kitaifa la Makanisa Kenya, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Kenya, Muungano wa Makanisa la ya Kiavenjelisti Kenya na Baraza Kuu la Waislamu Kenya.