Habari za Kitaifa

Daktari Laban Kiptoo azikwa, familia yadai kifo kilitokana na ushindani kazini

January 27th, 2024 2 min read

NA EVANS JAOLA

FAMILIA ya daktari wa Nakuru, Laban Kiptoo, aliyeuawa kinyama wiki jana, sasa inadai kwamba aliuawa na watu wanaomfahamu kutokana na ushindani kazini.

Wametoa kauli hii huku uchunguzi wa mwanapatholojia wa serikali, Dkt Titus Ngulungu, ukifichua kuwa daktari huyo alikufa kwa kunyongwa.

Familia hiyo sasa inataka hospitali iwajibike na kushirikiana na asasi za uchunguzi ndipo ifahamike kipi kilichojiri kabla ya mauti yake kutokea.

Vilevile, familia hiyo inataka serikali iharakishe uchunguzi ili waliomuua Dkt Kiptoo nao waadhibiwe vikali kisheria.

Hadi sasa, hakuna mshukiwa ambaye amekamatwa kutokana na mauti hayo ya kusikitisha.

“Tunashuku mauaji ya Dkt Kiptoo yalipangwa. Kwa hivyo, polisi watafichua sababu zilizofanya anyongwe,” akasema Leonard Kimtai, jamaa ya marehemu wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Familia ya marehemu ilisema kuwa wameridhishwa na uchunguzi huo wa upasuaji wa maiti ulioonyesha kuwa Dkt Lang’at alinyongwa mahali pake pa kazi.

Wakizungumza wakati wa mazishi ya Dkt Kiptoo shambani mwa babake eneo la Chematich, Cherangany, Kaunti ya Trans Nzoia mnamo Jumamosi, familia ilimrejelea marehemu, 6, kama mtu mchapakazi aliyekuwa na nidhamu mno.

Pia familia ilisema kifo chake sasa ni pigo kuu kwao kwa sababu ndipo tu alikuwa ameanza kukwea ngazi ya ufanisi.

Waliohudhuria mazishi yake nao walimrejelea kama mtaalamu ambaye alikuwa mwerevu mno na aliwahudumia watu kwa moyo wa dhati.

Kati ya waliohudhuria mazishi hayo ni madaktari, wenzake kazini na wanafunzi wa kozi za sekta ya utabibu kutoka Nakuru.

“Tumesikitishwa kuwa uchunguzi unachukua muda sana hata baada ya upasuaji wa mwili na uchunguzi wa kufanyika. Mwanetu aliuawa ndani ya hospitali ambako alikuwa akifanya kazi. Tunashangaa kwa nini inachukua muda sana kwa waliomuua kupatikana ilhali hospitali ilikuwa na vifaa vyote vya kiusalama,” akasema Bi Sara Rono, mamake marehemu.

Dkt Kiptoo alikuwa akihudumu katika Hospitali ya Nakuru ambapo alikuwa akiendelea na mafunzo yake ya kazi. Hasa alikuwa akiwajibikia kitengo kinachowahudumia wagonjwa mahututi.

Dkt Leonard Lang’at, nduguye marehemu ambaye anafanya kazi Turkana, alisikitika kuwa nia ya mauaji ya nduguye bado haijulikani.

Alitoa wito kwa asasi za uchunguzi kuzama na kuibuka na jibu kwa familia hiyo kuhusu aliyemuua mwanao.
“Ndugu yangu alikuwa mtu tulivu na tunajua hakuwa na tatizo na mtu yeyote. Yeye si mchokozi na kifo chake ni pigo kuu kwetu,” akasema Bw Lang’at.

Dkt Kiptoo alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Egerton Februari 2023 baada ya kusomea kozi ya matibabu na upasuaji. Alipata alama za juu zaidi (first class) na baada ya kufuzu alijiunga na Hospitali ya Nakuru kwa mafunzo ya kazi.

Marehemu alizaliwa mnamo 1977 na alikuwa mtoto wa nne kwenye familia ya watoto watano.

Mwili wake ulipatikana na maafisa wa usalama ukiwa hauna majeraha yoyote kando na alama kidogo kidogo ishara kuwa alikuwa akipambana kujinasua.

Kizungumkuti katika uchunguzi ni kuwa kamera za CCTV za hospitali zilikuwa zimeharibika na imekuwa vigumu kufuatilia yaliyojiri siku ya mauti yake.