Dalili Klopp yuko karibu kuagana na Liverpool

Dalili Klopp yuko karibu kuagana na Liverpool

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amekiri kwamba anapitia mmojawapo wa misimu migumu mno, ya kufikirisha sana na ya kusikitisha zaidi katika kipindi cha miaka 20 ya taaluma yake ya ukufunzi.

Hii ni baada ya Liverpool kupoteza mechi yao ya sita mfululizo ligini ugani Anfield kwa kulazwa 1-0 na Fulham mnamo Machi 7, 2021. Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Fulham kujivunia uwanjani Anfield tangu 2012.

“Vijana wana ari ya kushinda lakini hatufungi mabao ya kutuzimia kiu hiyo. Inatulazimu kutafuta mbinu nyingine ya kubadilisha mambo,” akatanguliza Klopp.

“Si lazima kila mara nijivunie mafanikio katika taaluma hii. Lakini hali ya sasa ya kikosi inasikitisha ikizingatiwa ubora wa kampeni tulizokuwa nazo muhula uliopita. Huu ni msimu mbaya zaidi katika taaluma yangu ya ukocha,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Ujerumani katika kauli iliyodokeza uwezekano wake wa kuagana na Liverpool hivi punde.

Iwapo ataondoka Liverpool, Klopp anapigiwa upatu wa kutua Real Madrid ambao watakuwa radhi kumtimua Zinedine Zidane ikiwa atashindwa kuwanyanyulia miamba hao wa Uhispania taji lolote msimu huu.

Hata hivyo, gazeti la La Gazzetta dello Sport nchini Italia limedokeza uwezekano wa Klopp kusajiliwa na Bayern Munich iwapo kocha Hansi Flick atashawishika kukubali mikoba ya timu ya taifa ya Ujerumani ikiwa Joachim Loew atapigwa kalamu kwa sababu ya matokeo duni.

Hii si mara ya kwanza kwa Klopp, 53, kushuhudia kikosi chake kikisuasua baada ya kujivunia ufanisi mkubwa katika msimu uliotangulia.

Kocha huyo aliwahi kuongoza Borussia Dortmund ya Ujerumani kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo 2010-11 na 2011-12.

Hata hivyo, Dortmund walikamilisha kampeni za 2012-13 katika nafasi ya pili kwa alama 66 huku pengo la pointi 25 likitamalaki kati yao na Bayern Munich waliotwaa ufalme. Klopp aliagana na Dortmund mnamo 2014-15 baada ya kikosi chake kuambulia nafasi ya saba jedwalini na akapokezwa mikoba ya Liverpool mnamo Oktoba 2015.

Chini ya Klopp, Liverpool walitinga fainali ya UEFA mnamo 2018 ila wakazidiwa ujanja na Real Madrid ya Uhispania kabla ya kutawazwa mabingwa wa kipite hicho msimu uliofuata baada ya kubwaga Tottenham.

Mnamo 2019-20, Liverpool walitwaa taji la EPL baada ya mechi 31 pekee na wakavunja rekodi ya kunyanyua ubingwa wakisalia na idadi kubwa zaidi ya michuano ya kusakata.

Huku ushindi wa Fulham ukiweka hai matumaini yao ya kusalia ligini msimu ujao, matumaini ya Liverpool kumaliza kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya UEFA mnamo 2021-22 yalididimia zaidi.

Liverpool walinyanyua taji la EPL msimu uliopita wa 2019-20 wakijivunia pengo la alama 18 kati yao na Man-City walioambulia nafasi ya pili. Hadi Liverpool walipopigwa na Burnley mnamo Januari 2021, miamba hao wa soka ya Uingereza hawakuwa wamepoteza mechi yoyote ya nyumbani kutokana na mapambano 68 ya EPL.

Hadi walipovaana na Fulham, Liverpool walikuwa michuano dhidi ya Brighton, Man-City, Everton na Chelsea uwanjani Anfield.

Mabingwa hao watetezi ambao kwa sasa hawajashinda mchuano wowote kati ya minane iliyopita, sasa wanakamata nafasi ya nane kwa 43, saba nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora. Liverpool ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kupoteza jumla ya mechi sita mfululizo za EPL katika uwanja wao wa nyumbani baada ya Huddersfield Town mnamo Februari 2019.

Aidha, Fulham ndicho kikosi cha kwanza limbukeni katika EPL kuwahi kushinda Liverpool ligini ugani Anfield tangu Blackpool wafanye hivyo mnamo Oktoba 2010 chini ya kocha Roy Hodgson.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ndoa ya BBI yaingia doa

Auka Gecheo ataka Kenya kufanya zaidi kufikia Uganda kwenye...