Jamvi La Siasa

Dalili Waiguru alenga unaibu kwa Ruto 2027

May 26th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru amewaacha wengi vinywa wazi kwa kujiunga kwenye tapo la viongozi wa Mlima Kenya wanaomshambulia Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye kinyang’anyiro cha ubabe wa kisiasa Mlima Kenya.

Bi Waiguru, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Jumatatu alimshutumu Bw Gachagua kwa kuendeleza kampeni ya kudumaza ndoto za kisiasa za viongozi kutoka Mlima Kenya, akisema kitendo ni kinyume cha Katiba na misingi ya kidemokrasia.

Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Bi Waiguru anayehudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, alisema hivi: “Maafisa wa umma kama wale wanaoshikilia nafasi ya naibu rais hawapaswi kuzichukulia kama mali ya kibinafsi. Ni makosa kwa mtu kuwataka Wakenya kuamini kuwa ni mwiko mwa mtu yeyote kuwa na ndoto ya kuwa naibu rais.”

Akaongeza: “Japo tunaheshimu afisi ya Naibu Rais, sawa na afisi zingine za uongozi, demokrasia endelevu haituruhusu sisi kama washikilizi wa afisi hizi kuzichukulia kama za kibinafsi kiasi kwamba inaonekana kama mwito kwa mtu mwingine kuwa na ndoto za kuzishikilia. Tunazishikilia afisi hizo kwa niaba ya wananchi, sio kama wamiliki wazo.”

Gavana huyo wa Kirinyaga alisisitiza kuwa kila Mkenya, wakiwemo wanawake na vijana, wako na haki na kuendeleza ndoto zao za kushikilia nyadhifa zozote za uongozi nchini Kenya.

Kauli ya Gavana huyo, kulingana na wadadisi, inaashiria kuwa amejitosa kwenye ulingo wa kung’ang’ania nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ni wazi kwamba sasa Bi Waiguru amejiunga kwenye orodha ya wanasiasa wa Mlima Kenya wanaopania kumpiga Gachagua kumbo ili ateuliwe mgombea mwenza wa Rais Ruto angetaka kubadilisha mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2027. Awali, ilidhaniwa kwa Bw Ndindi Nyoro ndiye alikuwa akiimezea mate nafasi hiyo,” anasema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi.

Hujumu Gachagua

Kauli ya Bi Waiguru ilijiri siku moja baada Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kuonya kuhusu kile alichokitaja kama njama inayoendelezwa na viongozi fulani kumhujumu Bw Gachagua katika serikali ya Kenya Kwanza.

Akiongeza Jumapili katika eneobunge la Kieni kaunti ya Nyeri, Gavana huyo alidai kuwa kuna viongozi fulani kutoka Mlima Kenya wanaotumiwa “na watu wengi” kuchochea uhasama kati ya Naibu Rais na bosi wake, Rais William Ruto.

Hatutakubali

“Hatutakubali jambo kama hili ambalo litapelekea Bw Gachagua kupitia mateso ambayo Ruto alipitia wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta,” akasema.

Kwa muda sasa, Bw Nyoro ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti, ndiye alionekana kuwa “tishio” kwa Bw Gachagua katika hamu ya kuendelea kushikilia wadhifa wa Naibu Rais endapo Rais Ruto ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Lakini kulingana na Bw Mokua, hatua ya Bi Waiguru kujiweka katika orodha ya wanasiasa wanaodhaniwa kumezea mate nafasi ya Gachagua ni mkakati wa kumfanya aonekane kama “nabii asiyethaminiwa nyumbani”.

“Aidha, huenda Bi Waiguru anajipanga kwa nafasi hiyo kufuatia dokezo la Rais Ruto kuwa miaka ijayo wagombea urais wanapaswa kuwateua wanawake kama wagombeaji mwenza ili kuwaweka akina mama karibu na uongozi wa taifa,” anaeleza.

Kulingana na Katiba, magavana, sawa na Rais, hawaruhusiwi kushikilia wadhifa huo kwa zaidi ya mihula miwili.

Hii ndio maana sasa Bi Waiguru kujipanga kwa nafasi nyingine ya uongozi baada ya kukamilisha muhula wake wa pili 2027.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru. PICHA | MAKTABA