Makala

Dalili za ugonjwa wa kisukari

October 21st, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

KISUKARI ni ugonjwa wa kimetaboliki ambao husababishwa na ama kiwango cha juu kupindukia cha sukari au cha chini kabisa kwenye damu.

Insulini ni homoni ambayo huruhusu na kufanya usawazisho wa kiwango cha sukari.

Insulini husababisha sukari kutoka kwenye damu ndani ya seli zako kuhifadhiwa au kutumika kwa nishati. Kwa ugonjwa wa kisukari, mwili wako hufanya insulini ya kutosha au haiwezi kutumia insulini kwa ufanisi.

Sukari ikizidi au ikipungua huathiri na kuharibu insulini ambapo kongosho hushindwa kuzalisha insulini kiwango kinachohitajika mwilini. Kutokana na sukari ya juu ya damu kutokana na ugonjwa wa kisukari huweza kuharibu mishipa yako, macho, figo, na viungo vingine.

Ili kuweza kutambua kama umeugua ugonjwa wa kisukari unatakiwa kujua dalili za awali za ugonjwa huo ambazo ni:

Kukojoa mara kwa mara

Ugonjwa wa kisukari unasababisha sukari kutolewa kwenye njia ya mkojo. Sukari inapotolewa, huambatana na maji hivyo kumfanya mgonjwa ajihisi upate mkojo kila mara.

Kuhisi kiu mara kwa mara

Unapokuwa na kisukari unapoteza maji mengi kupitia kwenye mkojo hali hii husababisha kupata mkojo mara kwa mara.

Kusikia njaa kali kila mara

Mwili unapoteza uwezo wa kutumia sukari katika kazi zake. Hali hii hufanya mwili wako kuhisi kuwa hakuna chakula cha kutosha. Hii ndio sababu inakufanya kuhisi njaa kila mara na hata baada ya kula unaendelea kuhisi njaa.

Uchovu wa mwili

Hii hutokana na mwili kushindwa kutumia sukari kutengeneza nishati ya kuwezesha mwili kufanya kazi zake.

Kupoteza uzani na kukonda

Ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezo wa mwili kuhifadhi sukari kwenye misuli. Hivyo mwili wako utaanza kupoteza uzito na kuanza kukonda.

Kulingana na Dkt Victor Achoka, wagonjwa wa kisukari wanaweza kuishi vyema kwa kuwa waangalifu sana na wanachokula, wafanye mazoezi ya kutosha na pia ufuatiliaji wa kibinafsi kwa kutumia chombo kiitwacho glucometer.