Dalili za upungufu wa maji katika ngozi

Dalili za upungufu wa maji katika ngozi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

KUNA tofauti ya ngozi iliyokosa maji na ngozi kavu.

Ngozi iliyokosa maji ni ile ambayo imesababishiwa hali hii na mambo ya nje kama kutokula vyakula vyenye afya na mtindo wa maisha kama unywaji wa pombe na kahawa mara kwa mara. Yote haya husababisha kupunguka maji kwenye ngozi yako na kuipa ngozi mwonekano hafifu.

Ngozi kavu hii hutokana na mambo asili ambapo inaweza kuwa umerithi au kuzaliwa nayo. Hali hii haiwezi kubadilika ila unaweza kuiboresha kwa kutumia bidhaa zinazoendana na ngozi yako.

Ishara za kuwa na upungufu wa maji katika ngozi ni nyingi.

Ngozi kuwasha

Ngozi inapokuwa kavu inajivuta na hii husababisha mwasho. Inawezekana ikawa kila mara baada ya matembezi, kuwa nje kwenye jua kali au hata upepo unafanya ngozi yako iwashe. Basi jua hii hutokana na kupungua kwa maji katika ngozi.

Kuongezeka kuwa nyeti

Ishara kubwa ya ngozi yako kuhitaji maji ni kuwa nyeti, na hii hutokana na kwamba vizuizi vya unyevu vimepungua kwa hivyo ulindaji wa ngozi yako kutokana na madhara ya nje umepungua. Bakteria na uchafu wa kawaida unaweza kuingia katika ngozi yako kwa urahisi na kusababisha ngozi ibadilike na kuwa nyeti zaidi.

Ngozi kuwa na mwonekano dhaifu

Kama ngozi yako inaonekana kuwa dhaifu au kuchoka basi hiyo ni ishara nyingine ya kwamba ngozi yako inahitaji maji. Ukosefu wa maji mwilini huathiri uwezo wa ngozi yako kufanya kazi muhimu. Bila unyevu wa kutosha, ngozi haitoi safu yake ya nje mara kwa mara lakini hii husababisha seli zilizokufa kujilimbikiza katika ngozi yako. Hii husababisha kuziba kwa mashimo na ngozi kuonekana dhaifu.

Mikunjo ya uzee

Ngozi iliyokosa maji huwa na mtindo wa kuzeeka mapema, angalia kwenye ngozi iliyozunguka macho yako, kama una mikunjo ambayo inaonekana inawezekana ni kutokana na ngozi kukosa maji. Unaweza kujua ngozi yako haina maji kwa kujifinya mashavu, kama itatokea laini basi moja kwa moja ngozi yako inaupungufu wa maji.

Ufanye nini ili kuondokana na tatizo hili?

Kunywa maji mengi

Kitu cha kwanza ambacho unatakiwa kufanya baada ya ngozi yako kukosa maji ni kuongeza maji. Kadhalika, unatakiwa kutumia bidhaa zenye unyevu ndani yake.

Epuka utumiaji wa mvinyo na kahawa

Hapa sio kwamba usinywe au uache kabisa bali ni kupunguza utumiaji wake. Kunywa vikombe viwili vya kahawa au glasi moja ya pombe kwa siku ni sawa kwa wenye mazoea na uraibu lakini kutumia vitu hivi mara nyingi kupita kiasi huharibu afya ya ngozi yako.

Oga au osha uso kwa kutumia maji ya ufufutende

Haya ni maji sahihi kuoshea uso wako. Yanaondoa uchafu vyema lakini pia yanasaidia kuhifadhi mafuta yako ya asili ya ngozi.

You can share this post!

Shanzu United FC yadondosha alama tatu dhidi ya wenyeji...

Fernandinho atia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja kambini...