Habari Mseto

Dan Wema: Pesa ninazowapa watu mitandaoni si za uhalifu

May 4th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

Dan Wanyonyi maarufu Dan Wema ni mhisani, mhubiri na mtayarishi wa vipindi vya mitandao ya kijamii.

Mwaka mmoja uliopita, Dan hakuwa na nyayo katika majukwaa ya kidijitali hadi alipoanza kuwatia watu majaribioni kubaini kama wana nyoyo za utu.

Kwa desturi, Dan hujifanya mhitaji ambaye pengine amekosa nauli akaona afadhali aombe watu wamsaidie.

Iwapo utamsaidia, mhubiri huyu huwarejeshea hela walizotoa na kuwazidishia pesa zaidi ama msaada wa aina nyingine.

Huwa si kazi rahisi na humhitajika kuwa jasiri kwa sababu wakati mwingine Bw Wema huwaomba watu ‘maskini’ hela.

Baadhi yao huingiwa na mori na kuzua vita kadri mhisani huyu anavyozidi kuwaomba msaada licha ya wao kusema hawana kitu.

Amewahi kuvurugwa na wafanyakazi wa mijengo waliouliza, “Kati yetu na wewe nani anafaa kuomba msaada?”

Baada ya hapo sokomoko ikaibuka kabla ya hali kutulizwa.

“Kusingekuwa na mtu wa kuingilia kati hata ningepigwa,” alikiri Bw Wema.

Kuna wakati mmoja Wema alimjaribu mhudumu wa bodaboda ampeleke hospitali ya Rufaa ya Moi Eldoret bila malipo.

“Ninahitaji kumwona mama yangu hospitalini; niko hapa na dada na kaka yangu, unaweza kutupeleka bila malipo?” aliuliza na kukubaliwa baada ya wengine kumkwepa.

“Nilihisi vizuri sana kujua kuwa watu wazuri bado wapo,” aliongeza.

Anatoa wapi pesa kuwapa watu?

Maswali yameibuka miongoni mwa watumiaji mitandao wanaodhani pengine Bw Wema anafanya biashara haramu kama za kusafisha pesa.

“Kuna baadhi ya watu wanasema ni pesa za ufisadi ambazo ninasafisha kwa kujifanya mhisani. Wengine hata wanakataa pesa zangu wakisema ninawasajili katika dhehebu la kuabudu shetani,” alisema.

“Pesa hizi zinatoka katika huduma yangu ya injili nyingine zikitoka kwa wahisani wanaojitolea kuendeleza mipango ya kusaidia jamii,” akaongeza.

Akizungumza na Podkasti ya Dau la Maisha, Dan alifichua mpango wake wa kuanza wakfu wa kusaidia jamii.

Kujibu tuhuma dhidi yake, mhubiri huyu maarufu kwenye mitandao ya TikTok alieleza pia kuwa yeye hujishughulisha na kilimo kama njia moja ya kutega uchumi.

Anavuna pesa katika mitandao ya kijamii

Mbali na kuendeleza mpango wa kuwajaribu watu kama wana nyoyo za utu, Bw Wema kadhalika hurekodi matukio na kupakia mitandaoni.

Anaeleza kuwa hubidi kupata idhini ya kuchapisha video hizo kwenye majukwaa dijitali kuepuka mizozo baadaye.

Alifichua pia kuwa kawaida anapata angalau Sh70,000 kutoka kwa mtandao wa YouTube kila mwezi.

“Hata mtandao wa TikTok pia hunipa hela wakati watumiaji walio katika mtandao huo wa video wananitumia zawadi,” Wema alipasua mbarika akisema amewahi kupokea Sh80,000 kutoka kwa wahisani wengine.