Michezo

Dani Alves ahusishwa na uhamisho kujiunga na Arsenal

July 16th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA mlinzi matata wa Mabingwa wa Ligue 1 ya Ufaransa Paris Saint Germain Dani Alves, amefichua kuwa klabu atakayojiungana nayo msimu unaoanza mwezi Agosti itatwaa mataji kadhaa, huku akiendelea kuhusishwa na kutua kambini mwa Arsenal.

Duru zinaarifu kwamba Arsenal maarufu kama The Gunners imeamua kumsajili beki huyo raia wa Brazil ambaye sasa hawajibiki timu yoyote baada ya mkataba wake na PSG kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita wa Ligue 1 2018/19.

Alves ambaye aliwahi kunolewa na kocha wa Arsenal Unai Emery akifunza kikosi cha PSG, inadaiwa yupo tayari kujiunga na mojawapo ya klabu zinazoshiriki Ligi ya Uingereza(EPL) ila anasisitiza klabu hiyo lazima itashinda mataji msimu wa 2019/20.

“Kwa sasa nipo huru japo bado nina malengo mengi ya kutimiza kwenye taaluma yangu ya soka. Kile ninaweza kusema ni kwamba klabu itakayobahatika kutwaa huduma zangu, itaibuka mshindi wa mataji mengi,” akasema beki huyo ambaye pia aliwahi kusakatia Juventus na FC Barcelona.

Nia ya Arsenal ambayo imeandaa bajeti ya Sh5 bilioni kugharimia ununuzi wa wachezaji wapya kumsajili beki Kieran Tierney wa Celtic kwa kima cha Sh3.8 bilioni imegonga mwamba baada ya klabu hiyo kukataa kiwango hicho cha fedha.

Klabu hiyo kutoka jiji la London pia imekuwa ikionyesha juhudi za kumleta ugani Emirates winga wa Crystal Palace Wilfried Zaha ambaye bei yake inakadiriwa kuwa Sh11 bilioni, ila juhudi hizo bado hazijafanikiwa.