Habari Mseto

Daraja hatari hofu kwa wakazi

April 25th, 2019 1 min read

NA JUSTUS OCHIENG’

WAKAZI wa Chiga na Kibos, Kaunti ya Kisumu, wanaishi kwa hofu daraja la Kibos kuporomoka.

Daraja hilo linalounganisha vijiji vya maeneo hayo na mji wa Kisumu liko katika hali mbaya, na ni hatari inayowakodololea macho wakazi.

Daraja hilo linaweza kuporomoka wakati wowote baada ya msingi wake kulegezwa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumatatu na kusababisha Mto Kibos kufurika.

Hata hivyo, baadhi ya wenyeji wamekashifu watu wanaozoa mchanga kando ya daraja hilo ambalo pia linaunganisha maeneobunge ya Muhoroni na Kisumu Mjini Mashariki, kwa kuchangia hatari hiyo.

“Mvua kubwa siku ya Jumatatu ilisababisha hasara zaidi kwa kuwa watu huzoa mchanga kando ya daraja hili kila mara,” akasema mkazi , Bw Peter Odongo. Daraja hilo pia huunganisha mji wa Kisumu na Gereza la Kibos, Kampuni ya Sukari ya Kibos, na maeneo mengine.

“Daraja hili huenda likasababisha vifo kwa kuwa matrela na mabasi yanayoelekea miji ya karibu hupitia hapa. Wizara ya Barabara inafaa kulikarabati kabla mauti hayajatokea,” akasema Bi , Anne Otieno, ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, Naibu Kamishna wa Kisumu Mashariki, Bi Josephine Ouko amesema wanashughulikia suala hilo.