Habari

Daraja jipya Krismasi ya mapema kwa watumiaji wa kivuko Mombasa

December 4th, 2020 1 min read

MOHAMED AHMED na MISHI GONGO

SERIKALI inatarajia kufungua rasmi daraja la Liwatoni, Kaunti ya Mombasa kabla ya sikukuu ya Krisimasi.

Akizungumza na wanahabari Ijumaa katika eneo la Liwatoni alipokuwa anakagua daraja hilo lililogharimu Sh1.9 bilioni, Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alisema ujenzi wake umefikia asilimia 92.

“Tunatarajia Rais Uhuru Kenyatta kufungua daraja hili kabla ya sikukuu ya Krisimasi. Leo hii tumekuja kulikagua kabla lifunguliwe rasmi,” akasema Bw Macharia.

Daraja hilo litakalotumiwa na watu pekee sasa limebakia asilimia nane pekee kukamilika.

Lilianza kujengwa Agosti mwaka huu na linatazamiwa kupunguza msongamano kwa kiasi kukubwa katika kivuko cha Likoni feri.

Waziri alieleza kuwa daraja hilo lenye upana wa mita sita litaruhusu watu kutokaribiana wanapovuka, hivyo kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema pia litakuwa na uwezo wa kuvusha ambulensi wakati wa dharura.

Bw Macharia aliongezea kuwa wanafanya majadiliano kuona iwapo baiskeli pia zitatumia daraja hilo.

Daraja hilo lenya urefu wa mita 715 linaelea kutoka eneo la Liwatoni mjini Mombasa hadi eneo la Ras Bofu maarufu kama Peleleza, Likoni.

Kwa mujibu wa Bw Macharia, meli kubwa kabisa huwa na urefu wa mita 50, kwa hivyo wajenzi wa daraja hilo walihakikisha wameacha nafasi ya kutosha kuwezesha meli kubwa zaidi kupita chini yake.

Alisema daraja hilo ni la muda tu ili kupunguza msongamano katika kivuko cha Likoni feri wakisubiri kujengwa kwa daraja la kudumu.

“Daraja la kudumu litakapokamilika, hili litang’olewa na kupelekwa Kaunti ya Lamu ama sehemu nyingine yoyote ambayo itakuwa na hitaji,” akasema Bw Macharia.

Alieleza kuwa daraja la kudumu litagharimu Sh210 bilioni na limepangiwa kuanza kujengwa Juni 2021, na kukamilika baada ya miaka mine.

Wakazi katika eneo la Likoni walipokea ujenzi wa daraja hilo kwa hisia mseto, baadhi yao wakifurahia uwepo wake huku wengine wakisema halitakuwa na manufaa kwao. Wengi walilalamika kuwa kufikia daraja hilo kutakuwa changamoto kwa kuwa ni mbali na steji za matatu wanazotegemea.