Habari Mseto

Daraja la aibu lililojengwa kwa mabati 

April 16th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI 

DARAJA la Nyamache, lililofanya baadhi ya wakazi wa eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii kuandamana Jumatatu, Aprili 15, 2024 lilianguka mwezi Mei mwaka jana, 2023.

Daraja hilo ndilo lililokuwa likitumiwa sana na yeyote aliyetaka kuingia Nyamache kwa kutumia miguu au magari.

Ni la kikoloni na lilijengwa miaka ya zamani kwa kutumia mabati na vyuma ambavyo sasa vimezeeka.

Kutokana na mvua kubwa ambayo aghalabu inashuhudiwa sehemu nyingi ardhi ya Gusii, daraja hilo lilisombwa na maji na kusababisha lami iliyokuwa ikipita juu yake kukatika.

Kwa muda huo wote, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitumia kivukio cha mbao, walichokitengeneza kupitia usaidizi wa diwani wao wa Masige Mashariki, Michael Motume.

Kufuatia kuporomoka kwake, raia wanaotafuta huduma za kiserikali katika afisi ya Naibu Kamishna wa eneo hilo, wamekuwa wakizunguka mji wa Nyamache kutumia barabara zingine ndiposa wahudumiwe.

Pia, wanafunzi wa chuo cha mafunzo ya utabibu cha Nyamache wamekuwa wakipata ugumu kuhudhuria masomo yao.

Magari ya kusafirisha majani chai kwenda kiwanda cha Nyamache pia yamekuwa yakikwama katika barabara za ndani kunaponyesha kwa kuwa daraja hilo muhimu lilianguka.

Ili kushinikiza washikadau kulikarabati kwa haraka, diwani Michael Motume na mwenzake wa Masige Magharibi Jacob Bagaka waliongoza maandamano ya amani kuonyesha kutoridhishwa kwao.

Daraja hilo ndilo linalotenganisha maeneo wakilishi ya Masige Mashariki na Masige Magharibi.

Wakiwa wamebeba mabango, waandamanaji hao walimtaka mbunge wa Bobasi Innocent Obiri kuweka presha kwa mamlaka inayohusika na ujenzi wa daraja hilo haraka iwezekanavyo.

“Ni aibu katika karne hii, bado kungali na daraja lililoundwa kwa mabati. Vifaa vilivyotumika ni vya kikoloni,” akalalamika Bw Motume.

Walimpa Mbunge Obiri siku 14 kuwapa majibu la sivyo watarejelea maandamano yao.

Baada ya kuandamana Nyamache yote kwa saa nyingi Jumatatu asubuhi, raia hao walitaka kuingia katika afisi za mbunge huyo kuwasilisha malalamishi yao.

Lakini maafisa wa polisi waliokuwa wamekita kambi katika makao hayo makuu, waliwarushia gesi ya vitoa machozi waandamanaji hao walipoanza kutikisa lango la kuingia humo.

Raia hao walitawanyika baada ya gesi hiyo kuwalemea.

Eneo la Kisii ni baadhi ya sehemu humu nchini zenye madaraja mabovu.

Mapema mwaka huu, mcheshi Eric Omondi alichangisha pesa zilizotumika kwa ujenzi wa daraja moja eneobunge la Bomachoge Chache, baada ya video ya mtoto aliyehatarisha maisha yake kwa kuvuka mto uliofura kusambaa mitandaoni.

Mtoto huyo alionekana akitumia daraja kuukuu la miti akienda shuleni, jambo lililowagusa watumiaji wa mitandao ya kijamii.