Habari za Kaunti

Daraja la kisasa lajengwa Mutituni kuepushia wakazi balaa ya mafuriko

January 29th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

WAKAZI wa lokesheni ya Mutituni katika Kaunti ya Machakos wamepata afueni baada ya Gavana Wavinya Ndeti kushirikiana na mbunge wa Machakos Mjini Caleb Mule kuzindua ujenzi wa daraja jipya.

Tayari matingatinga na malori yako katika eneo la Inyooni ambako wahandisi na vibarua wameanza kujenga nguzo za daraja jipya.

Sehemu kubwa ya eneo tambarare ya Inyooni huwa ni kawaida yake kuvurika baada ya mto Inyooni kutopitika kila mara kunaponyesha.

Hali hiyo huchangiwa na maji mengi ya mvua kutoka milima ya Iveti, Ngelani, Mua, Kisekini na Nduu ambayo husababisha kutopitika kwa mto huo.

Awali, kero la ukosefu wa kivukio cha magari na bodaboda ilishuhudiwa kwa muda mrefu na kusababisha wenyeji kulalamikia ofisi za serikali.

Hatimaye, kwa ushirikiano wa Gavana Wavinya Ndeti na Bw Mule, kazi ya ujenzi wa daraja la kisasa imeanza.

Hapo awali, sehemu ya barabara iliokosa daraja hilo haingepitika kwa sababu maji ya mafuriko yalikuwa yakisomba na kuvunja nyaya zilizotumika kujenga vizuizi vya maji na kuacha shimo kubwa ambalo lilikuwa hatari kwa usalama wa madereva wa magari na bodaboda.

“Wakulima sasa wanaweza kupeleka bidhaa sokoni na wenyeji wanaweza kupata huduma za matibabu, elimu na usalama kwa urahisi pindi daraja litakapokamilika,” chifu wa eneo la Mutituni Ancent Nzyoki alisema.

Barabara hiyo sasa imekarabatiwa na daraja hilo jipya linajengwa chini ya ufadhili wa serikali ya kaunti.

Kadhalika, daraja hilo ni muhimu kwani huunganisha maeneo ambako kunakuzwa kahawa, parachichi na mboga na soko la Muitituni, soko la Mavivye na soko kuu la Machakos.

Vilevile, linaunganisha vijiji kadhaa na huduma za serikali zikiwemo ofisi za machifu, hospitali sawia na shule na vituo vya polisi.