Makala

DARAJA LA MUNGU: Daraja la maumbile ya kiasili linalookoa wakazi Mai Mahiu wakati wa mafuriko

November 4th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa maeneo yenye barabara mbovu hutatizika sana wakati wa mafuriko kwa sababu shughuli za usafiri na uchukuzi huathirika vibaya.

Msimu wa mvua kubwa, sehemu kadha wa kadha nchini huangaziwa kutokana na mahangaiko ya uchukuzi, barabara kufurika na pia madaraja kusombwa na maji.

Kati ya mwezi Machi na Juni 2020, kando na kuwepo kwa janga la Covid-19, baadhi ya maeneo nchini yalishuhudia mafuriko yaliyosababisha mamia ya watu kuachwa bila makao na kupoteza mali ya thamani ya mamilioni ya pesa na wengine wakifariki.

Wakazi wa maeneo yaliyoathirika walionekana wakihangaika kusafiri kwa sababu ya barabara mbovu, mito iliyofurika na madaraja yasiyo na misingi thabiti kusombwa.

Licha ya eneo la Mai Mahiu kuwa nusu jangwa, katika kijiji cha Gishungu na ambacho hushuhudia ukosefu wa maji safi wakati wa ukame, wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia kuwepo kwa daraja la maumbile ya kiasili ambapo mwamba unawaokoa wakati wa mafuriko.

Mafuriko yanapobisha hodi, hayabagui endapo sehemu ni jangwa, nusu jangwa au hupokea mvua mara kwa mara.

Daraja hilo, maarufu kama Daraja la Mungu – ‘Darasha ya Ngai’ wanavyoita wenyeji – limekuwepo kwa muda mrefu, kulingana na wakazi.

“Mimi ni mzaliwa wa Mai Mahiu na nililipata likiwa pahala lilipo,” Mary Murage, 45, akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano katika daraja hilo.

Likiwa na urefu wa takriban mita 15 kutoka ng’ambo moja hadi nyingine, wenyeji wanahoji halikuundwa na yeyote. Ni la mwamba mkubwa, ambao chini yake ni pango ambalo Mto wa Kwanza (maarufu kama Rui rwa Mbere kwa mujibu wa wakazi) hupitia.

Aidha, ni pango kubwa linaloashiria mkondo unaoelekeza maji, kutoka sehemu ya juu kuelekea chini.

Daraja la Mungu – ‘Darasha ya Ngai’ wanavyoita wenyeji – eneo la Gishungu, Mai Mahiu limekuwa la manufaa kwa wenyeji wakati wa mafuriko. Mbwa akipita juu ya daraja lenyewe. Picha/ Sammy Waweru

Kulingana na Francis Njoroge, ipatayo miaka 10 hivi iliyopita, daraja hilo lilikuwa na upana mkubwa, ila baadhi ya magari yaliyojaribu kupitia juu yake yalilibomoa kandokando.

Kwa kuwa pikipiki hazina uzani mzito, wahudumu au wendeshaji hulipitia.

“Kwa hakika ni Daraja tulilotunukiwa na Mwenyezi Mungu na ndio maana huliita ‘Daraja la Mungu’. Ni la manufaa sana Mto wa Kwanza unapofurika,” Njoroge anaelezea.

Mkazi huyo anasema mvua ya mafuriko inaposhuhudiwa, sehemu za kingo za Mto wa Kwanza hufuja na kwamba kasi ya maji kwa vyovyote vile huwa haiyumbishi daraja hilo.

Kwa upeo wa macho, unaposimama juu ya daraja hilo, linaonekana kuwa na kimo kirefu, Francis Njoroge akisema ni zaidi ya futi 20, kuenda chini.

Kinyume na madaraja yanayotengenezwa na wanakandarasi, kwa mawe maalum ya ujenzi, saruji na kusitiriwa na vyuma, Daraja la Mungu, juu, ndani, chini na kandokando ni miamba. Isitoshe, kandokando limesitiriwa na miamba mirefu.

Mto wa Kwanza urefu wa karibu mita 100 kuanzia katika daraja hilo, nao pia una kuta za miamba, mkondo wa maji ukiendelea kuufanya kuwa mrefu kuenda chini.

Wakati wa ziara katika daraja hilo, licha ya kuwa ulikuwa msimu wa kiangazi, taswira ya mkondo wa maji iliashiria Mto wa Kwanza hufurika hadi pomoni, kutokana na michirizi iliyojichora kandkando kwenye miamba.

Wakazi wanasema pango la daraja hilo na mapango mengine katika Mto wa Kwanza ni makazi ya wanyama hatari wa msituni kama vile nyoka. “Kiwango cha maji kinapopungua au hata kuisha, nyoka hujitokeza wakitafuta maji na chakula,” akadokeza Precious Wambui, mkazi.

Fauka ya changamoto hiyo, wenyeji wanasema Daraja la Mungu lina faida chungu nzima hususan msimu wa mafuriko.

Huku wakilitaja kama raslimali waliyotunukiwa na Mungu, wanahimiza watalii kutoka humu nchini na nje ya nchi kuzuru eneo la Gishungu, Mai Mahiu kujionea darajahai hilo na ambalo ni la maajabu kutokana na ‘maumbile’ yake.

Daraja la Mungu – ‘Darasha ya Ngai’ wanavyoita wenyeji – eneo la Gishungu, Mai Mahiu limekuwa la manufaa kwa wenyeji wakati wa mafuriko. Picha/ Sammy Waweru

Ni hatua wanayoamini itachangia kukua na kuimarika kwa eneo hilo, kimaendeleo, kupitia ziara ya watalii. Bw Najib Balala ndiye Waziri wa Utalii, na wanahisi kutambuliwa kwa Draja la Mungu kama kivutio cha utalii, itakuwa ni kwa manufaa yao.

Maji ya Mto wa Kwanza yana uchachu wa chumvi, na kulingana na Wanajiografia ni hali inayochangia kuchimbika kwa miamba kwenye mito kuunda mapango.

Vilevile, kasi ya maji kwa muda mrefu husababisha kuwepo kwa mashimo kwenye miamba na hatimaye kuunda pango.

Yote tisa, kumi ni jukumu la wataalamu wa Jiografia na pia Wanasayansi kujituma eneo hilo na kuweka mambo paruwanja daraja la aina hiyo kuibuka.