Habari Mseto

DASH 100 Bombardier: FlySax yarejelea safari zake Kitale

June 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya ndege ya FlySax, tawi la Fly540, imerejelea safari zake za Kitale baada ya zaidi ya majuma mawili, tangu ajali mbaya ya ndege yake Juni 5, ambayo ilipelekea vifo vya watu 10.

Ndege hiyo ilirejelea safari zake Alhamisi ambapo kurejea kwa huduma zake kulipokelewa vyema na wateja wake.

FlySax ilitoa ndege kubwa, DASH 100 Bombardier, kwa ziara kati ya Wilson na Kitale.

Ndege iliyoanguka Aberdares FlySax  5Y-CAC ilikuwa ikiendeshwa na Barbara Kamau, 28 na Jean Mureithi.

Ndege DASH 100 ambayo ina nafasi 37 za abiria itakuwa ikimaliza safari kati ya Nairobi na Kitale katika muda wa dakika 50 ikilinganishwa na FlySax iliyoanguka ambayo ilikuwa ikichukua dakika 75 kati ya Nairobi na Kitale.