Makala

DAU LA MAISHA: Afisa wa afya anayekabili janga la uzazi wa mapema

November 16th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

TAKWIMU zinaonyesha kwamba idadi ya wasichana wanaoshika mimba na kuzaa wakiwa wangali wachanga imekuwa ikiongezeka hapa nchini.

Bila shaka ni jambo linalotisha sana na ndiposa huduma za watu kama Bi Violet Muinde zinahitajika.

Bi Muinde ni afisa wa afya na msimamizi wa mradi wa kituo cha kimataifa cha afya ya uzazi (ICRHK) katika kituo cha kiafya cha Mtwapa, Kaunti ya Kilifi ambapo kwa miaka miwili sasa amekuwa akishughulikia akina mama wachanga ambao wamekuwa wakizuru kituo hiki ili kupata usaidizi.

Kituo hiki kinachofadhiliwa na Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu UNFPA kimekuwa kikishughulikia kikundi hiki cha akina mama ambao mara nyingi hawajatimiza umri wa miaka 24.

Baadhi ya huduma zinazotolewa hapa ni pamoja na kuwafunza kuhusu mbinu za upangaji uzazi.

“Huduma hii ni muhimu hasa ikizingatiwa kwamba ni rahisi kwa akina mama hawa kushika mimba za pili na kuzaa watoto wengine kabla ya kutimu miaka 24, suala ambalo lina uwezekano wa kuwazamisha zaidi katika umaskini,” aeleza.

Aidha, huduma zao zimekuwa zikihusisha kuwapa akina mama hawa ushauri nasaha hasa kutokana na hali ngumu ya kimaisha inayotokana na kuzaa mapema. Hii ni hasa ikizingatiwa kwamba wengi wao huwa hawajakamilisha masomo, hivyo hawana taaluma wala ajira.

Pia, mara kwa mara akina mama hawa ambao huwalea wanao kivyao wamekuwa wakipokea msaada. “Msaada huu umekuwa ukihusisha nguo za watoto kwa wale wanaokaribia kuzaa, nepi na wakati mwingine nauli ya kuwawezesha kufika ili kupokea mafunzo.”

Mbali na hayo, msaada umekuwa ukihusisha ushauri wa kisaikolojia ambapo ni muhimu kwa wasichana hawa ambao mara nyingi hukumbwa na mafadhaiko hasa ikizingatiwa kwamba wao huwa wameachiwa mzigo wa kulea na wanaume waliowatunga mimba.

Ni shughuli ambayo tangu 2017 imenufaisha zaidi ya wasichana 2000 eneo hilo. Bi Fatuma Tsuma, ni mojawapo ya wanufaishwa wa mradi huu. Kutokana na huduma alizopokea kutokana na mradi huu, mwanafunzi huyu wa kidato cha tatu alirejea shuleni baada ya kujifungua.

Hii ilimfanya kuvunja rekodi na kuwa msichana wa kipekee kijijini mwake kurejea shuleni baada ya kushika mimba na kuzaa.

“Nilipopata mimba, niliendelea na masomo hadi mimba ilipofika miezi minane ambapo nilibaki nyumbani na kujifungua. Pindi mtoto alipotimiza umri wa miezi sita nilirejea tena shuleni mumo humo na kuendelea na masomo,” aeleleza.

Bi Sheila Maina, 22, pia ni mmojawapo wa wanufaika wa mradi huu.

“Niliachiwa mzigo wa kumlea mwanangu wa miaka miwili baada ya babake kutelekeza majukumu yake,” asema.

Mwanzoni, maisha yalikuwa magumu kwani hakuwa na mbinu ya kujikimu kimaisha.

“Lakini kutokana na ushauri nasaha niliopokea hapa, nilipata nguvu ya kuanzisha biashara ambayo japo haina kipato kikubwa, imenisaidia kukidhi mahitaji yangu na ya mwanangu,” asema Bi Maina.

Kulingana na Bi Muinde, ongezeko la idadi ya wasichana wanaozidi kushika mimba limewafanya kuanzisha kampeni za kueneza mafunzo ya uzazi na virusi vya HIV katika shule eneo hilo.

“Kufikia sasa tumefanikiwa kueneza mafunzo haya katika shule nne za msingi na upili eneo hili,” aongeza.

“Tabia ya kutegemea mfuko wa mwanamume ndio inawafanya iwe rahisi kwao kunaswa kwenye mtego huu, na sharti tuiangamize,” aongeza.