Makala

DAU LA MAISHA: Afunza watoto, vijana kuthamini mazingira safi

April 27th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

SIO siri kwamba ulimwengu unazidi kusakamwa na uchafuzi wa mazingira huku hasa janga la plastiki likizidi kuwa donda ndugu.

Hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Bi Zainab Ngari, 22, kujitosa katika shughuli sio tu za kuhamasisha jamii kuhusiana na athari za uchafuzi wa mazingira, bali pia yeye mwenyewe kuhusika vilivyo katika harakati za kukabiliana na tatizo hili.

Kwa miaka miwili sasa, Bi Ngari amekuwa akiendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira kupitia mradi wa Jewel Youth Foundation ambao umekuwa ukitekeleza shughuli zake hasa katika eneo la pwani.

Kinachofanya mradi huu kuwa wa kipekee ni kwamba anahusisha vijana na wanafunzi wa shule za msingi katika shughuli hii.

Wamekuwa wakiungana na mashirika mengine kufanya miradi ya kuhifadhi mazingira kama vile kupanda miti, na kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kupunguza matumizi ya plastiki miongoni mwa mambo mengine.

Pia, wamekuwa wakiendesha shughuli za usafi kwa kushirikiana na kitengo kinachosimamia fuo nchini.

Aidha, wamekuwa wakiandalia wanafunzi wa shule za msingi hafla za kuwaelimisha kuhusu mazingira kupitia mashindano ya uandishi wa insha, mashindano ya uchoraji, ushairi, nyimbo na densi ambapo mshindi anapokea tuzo.

“Tunawafunza kuhusu jinsi ya kuhifadhi mazingira kwa kudhibiti uchafu, vilevile upanzi wa miche na kuishughulikia. Kufikia sasa tumepanda zaidi ya miche 250 kwa ushirikiano na huduma ya misitu eneo la Kwale,” anaeleza.

Pia, wameshiriki mara nne katika shughuli za usafi katika maeneo ya pwani na jijini Nairobi.

“Mwaka 2018 tulishiriki katika hafla ya kimataifa ya usafi na hata kutambuliwa kwa ushiriki wetu na halmashauri ya uhifadhi wa bahari,” anaongeza.

Baadhi ya shule ambazo wamefanya nazo kazi ni pamoja na shule za msingi za Mkumbi na Ng’ombeni eneo la Kwale.

Sio hayo tu kwani pia wako mbioni kuanzisha shughuli za kuwagawia wasichana wa shule za msingi visodo vinavyoweza kutumika mara kadhaa.

“Kuhusiana na visodo, tunachanga fedha hasa kutoka kwa marafiki na wahisani mtandaoni na kununua visodo hivi, kabla ya kutambua wanafunzi wanaohitaji na kuwagawia,” anasema.

Saikolojia

Bi Ngari alianzisha mradi huu pindi baada ya kukamilisha elimu ya Chuo Kikuu mwaka wa 2017 ambapo alikuwa akisomea saikolojia.

“Kilichonisukuma ni kwamba baada ya chuo kikuu nilihudumu katika kituo cha urekebishaji tabia nyumbani kwetu eneo la Kirinyaga. Niligundua kwamba idadi kubwa ya vijana hawa walikuwa wameacha masomo wakiwa katika chuo kikuu kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya,” anaeleza.

Anasema kwamba ilimuuma sana kuona vijana ambao wangefaa kuwa wamekamilisha masomo yao, wakiwa wamekwama wametawaliwa na dawa za kulevya, na hivyo akaanza kutafuta mbinu sio ya matibabu bali kinga.

“Nilitaka kujihusisha na shughuli ambazo zingewafanya vijana kujihusisha na shughuli zingine zenye manufaa,” anaeleza.

Mbali na hayo, penzi lake katika masuala ya mazingira lilianza tokea utotoni huku ari yake ya kutaka kuleta mabadiliko ikichochewa na jinsi watu wengi walivyokuwa wakipuuza umuhimu wa mazingira.