Makala

DAU LA MAISHA: Anahamasisha mtoto wa kike kusomea sayansi

March 14th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

UFANISI wake kama mhadhiri, mtafiti na mtoa nasaha katika masuala ya sayansi ya kompyuta umemtambulisha sio tu humu nchini bali kimataifa.

Kutana na Dkt Chao Mbogo, mkuu wa kitivo cha Sayansi na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Kenya Methodist, KEMU.

Ufanisi wake katika masuala ya kielimu, uvumbuzi, vile vile mchango wake katika jamii vimemfanya kupokea tuzo mbali mbali humu nchini na mbali.

Kwa mfano, hivi majuzi alipewa tuzo ya 2020 OWSD-Elsevier Foundation Award kutokana na mchango wake katika uhandisi, ubunifu na teknolojia.

Aidha, mwaka wa 2015 alipokea tuzo ya Schlumberger Faculty for the Future award, ambayo iliwatambua wanawake katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati STEM.

Mwaka wa 2017 pia alitambuliwa kama mojawapo ya wavumbuzi katika tuzo ya Quartz Africa Innovators, huku mwaka wa 2018 akipewa tuzo ya uongozi ya Zuri award kutokana na mchango wake katika jamii.

Hizi ni baadhi ya tuzo ambazo zimepamba safari ya mojawapo ya wanawake wachache walio na shahada ya uzamifu katika masula ya Sayansi ya Kompyuta nchini.

Lakini licha ya kufanya vyema, Dkt Chao anasema kwamba mwanzoni haikuwa ndoto yake kujihusisha na fani hii.

“Babangu alikuwa mhadhiri katika chuo cha mafunzo ya ualimu huku mamangu akihudumu katika benki. Kwa upande wangu nilikuwa napenda hisabati sana ambapo nilikuwa na ndoto ya kujiendeleza na somo hili hata baada ya shule ya upili,” aeleza.

Na hii ndio sababu alidinda kuitika mwito wa kujiunga na chuo kikuu kusomea masuala ya chakula na lishe. Badala yake, aliamua kutuma maombi ya kusomea hesabu na sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha KEMU; uamuzi anaotaja kuwa muhimu sana maishani mwake.

Ni hapa ndipo msingi wake katika tasnia hii ulikuwa thabiti kwani mwishowe alihitimu na kiwango cha kwanza chuoni. Ni suala lililomshindia ufadhili wa kimasomo ambapo alisomea shahada yake ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza.

“Niliporejea nilianza kufunza sayansi ya kompyuta katika chuo changu cha zamani,” aeleza. Na haukuwa muda mrefu kabla ya jitihada zake kutambuliwa ambapo alichaguliwa na kuwa mkuu wa idara ya sayansi ya kompyuta, wakati huo akiwa na miaka 28 pekee.

“Nikiwa hapa ndipo nilianza kugundua mapengo miongoni mwa wanafunzi kwani hawakuwa na vifaa vya kutosha vya kusoma kozi hii. Hapa nilianza kujiuliza ni vipi ningewasaidia kutumia simu zao kujifunza?”

Ni wazo hili lililowasha moto wake wa kusomea shahada ya uzamifu. “Nilitaka kusuluhisha tatizo hili. Nilitaka kuelewa jinsi ya kusanifu upya majukwaa kwenye simu za rununu na hivyo kuwasaidia wanafunzi kujifunza vyema,” asema.

Kwa hivyo kupitia ufadhili wa Hasso Plattner Institute Fellowship, alijiunga na Chuo Kikuu cha Cape Town ambapo mwaka wa 2015 alihitimu na shahada yake ya uzamifu.

Baada ya kurejea nchini, alirejelea kazi yake ya uhadhiri chuoni na kuwa mkuu wa idara hadi mwaka wa 2018 alipopandishwa madaraka na kuwa mkuu wa kitivo cha sayansi na teknolojia katika taasisi hiyo.

“Sikumbuki nikifunza darasa lililokuwa na zaidi ya wanafunzi kumi wa kike. Kuna nyakati unapata mwanafunzi mmoja au wawili wa kike,” aongeza.

Hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma kuanzisha KamiLimu, jukwaa la unasihi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosomea saayansi ya kompyuta. Wamekuwa wakishirikiana na wataalamu katika sekta ya teknolojia huku mpango huu ukiwa na uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 wa wanafunzi wa jinsia zote mbili.