Makala

DAU LA MAISHA: Anawainua wazazi wanaolea peke yao

June 29th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

MARA nyingi wazazi wanaowalea wanao peke yao (single parents) hukumbwa na changamoto ya kutekeleza majukumu yao ya malezi, vilevile kukidhi mahitaji bila usaidizi.

Hiyo ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Amy Kyalo, kuanzisha Single Parents Initiative, mradi wa kusaidia wazazi wanaojipata katika masaibu haya.

Mradi huu wenye makao yake eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos, unanuia kusaidia wazazi hawa hasa kutoka sehemu za mashambani, ili kujihusisha na shughuli za kujitafutia riziki ya kuweza kukidhi mahitaji ya familia zao.

Kwa mwaka mmoja sasa amekuwa akifanya kazi na wazazi wanaowalea wanao peke yao.

“Mara nyingi wazazi hawa huwa wajane, wataliki au wameachana na wenzao kutokana na sababu zingine kama vile dhuluma za kinyumbani,” aeleza.

Kwa kawaida shirika hili husaidia wahusika kukuza vipaji vyao ili kuvitumia kujipatia fedha.

“Na kwa wale ambao hawana uhakika kuhusu ujuzi walio nao, tunawasaidia kutambua na kuukuza ili kujichumia pato,” aeleza.

Kulingana na Bi Kyalo, ujuzi huu waweza kuwa wa ukulima, ususi, upishi au biashara rejareja.

“Swali ambalo sisi huwauliza ni walicho nacho mikononi. Je, ni mali au ujuzi ambao tunaweza kukusaidia kuukuza na kuubadilisa ili kuwa biashara ya kuleta faida za kifedha?” aeleza.

Mara nyingi wamekuwa wakifanya hivi kwa kuwaunganisha wahusika na wataalamu katika nyanja mbalimbali za kibiashara na kitaaluma.

Bi Kyalo anasema kwamba kawaida wao hufanya kazi na wanaume na wanawake.

“Hata hivyo tumegundua kwamba, watu wengi wanaowasiliana nasi wakitaka usaidizi ni wanawake,” aongeza.

Kulingana naye mara nyingi wao hupata wazazi hawa kwa kuwasiliana na makanisa.

“Tumeamua kufanya kazi na makanisa kwani hapa ndipo huwa kimbilio la wengi walio na matatizo ya ndoa, ambapo mara nyingi huwa wamejaribu vilivyo kuokoa uhusiano wao bila mafanikio,” asema.

Kufikia sasa familia kadha zimenufaika kutokana na mradi huu.

“Tayari kuna familia tano ambazo zimenufaika kutokana na shughuli zetu za mafunzo. Aidha, nina kikundi cha wajane kutoka eneo la Machakos ninachosaidia kuanzisha miradi ya kujiundia riziki,” asema.

Bi Kyalo alianzisha mradi huu mwaka jana huku mambo kadha yakichangia uamuzi wake.

Kwanza, nilipata msukumo kutokana na mambo niliyopitia mwenyewe,” aeleza.

Lakini pia kichocheo kikuu kilikuwa kukabiliana na visa vya wazazi kuwaua wanao kutokana na ugumu wa maisha.

“Mzazi anayewalea wanawe peke yake huhitaji nguvu sana, ambapo mambo huwa mabaya zaidi hasa ikiwa hauna kipato. Ni masaibu ya aina hii yanayochangia visa vya wazazi kutekeleza maovu kuepuka shida hizi,” aeleza.

Aidha, nia yake ilikuwa kubadili dhana potovu kuhusu watoto wanaolelewa na wazazi wa aina hii.

“Tunaishi katika jamii ambapo watoto kutoka familia za aina hii huchukuliwa kuwa watovu wa nidhamu, na ambao baadaye hugeuka waraibu wa pombe, mihadarati au ukahaba. Mara nyingi si kweli na hivyo nia yangu ilikuwa kubadilisha mtazamo huu,” asema.

Lakini licha ya kuwa tayari uwepo wao umeanza kuhisiwa na wengi, changamoto hazikosi. “Changamoto kuu imekuwa kukabiliana na watu wenye nia mbaya. Mara kadha tumekumbana na wazazi wanaodanganya kuhusu hali yao ili kunufaika. Tunapoanzisha uchunguzi kubaini ukweli, hugeuka na kuwa wakali na hata kuzua vurugu, suala ambalo kidogo linatuvunja moyo,” aeleza.

Lakini Bi Kyalo asema hii haijazima azma yake. Nia yake kwa sasa ni kuwapa nguvu wazazi hawa na pia kusaidia watoto wao kukua kwa ujasiri bila kuhisi haya ya kulelewa na mzazi mmoja.