Makala

DAU LA MAISHA: Atumia taji la urembo kuboresha jamii yake

July 27th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

ANATUMIA urembo wake kuboresha maisha ya watoto wanaoishi na ugonjwa wa kiakili au Tawahudi (autism) hali ambapo mhusika huwa na matatizo ya mawasiliano na hata kukosa mbinu za uhusiano na wengine.

Kutana na Felister Kimotho, 18, Malkia wa Urembo wa Utalii yaani Miss Tourism, Kaunti ya Nyandarua mwaka wa 2019-2020.

Bi Kimotho amejitwika jukumu hili, kazi aliyoanza mapema mwaka huu huku akiendeleza shughuli zake hasa katika eneo la Nyandarua.

Huku akifanya hivi kwa usaidizi wa serikali ya Kaunti, kanisa, vijana na jamii kwa ujumla, jitihada zake zinahusisha kuhamasisha na kuwaelimisha wakazi kuhusu hali hii na kutafuta mbinu za kuwasaidia.

“Mafunzo yanahusisha ushauri nasaha kwa wazazi wa watoto hawa ili kuwanasua kutokana na dhana potovu kwamba hali hii inasababishwa na laana au ushirikina. Hii ni muhimu kwani inawapa moyo wa kuwashughulikia watoto wao wanaokumbwa na hali hii badala ya kuwaficha,” aeleza.

Aidha, husaidia wazazi wa watoto hawa kupata nafasi katika shule za walemavu, kupata kadi za utambulisho za ulemavu, vile vile kuwapa jukwaa la kuwasilisha changamoto wanazokumbana nazo kila siku.

“Kwa kufanya hivi inakuwa rahisi kuwasajili na hivyo kuwawezesha kupata msaada,” aeleza.

Kadhalika huwapa ushauri watoto hawa na pia kuwatafutia ufadhili kutoka kwa serikali za kitaifa na kaunti.

“Nimekuwa nikikutana na maafisa wa serikali, vile vile kuungana na marafiki zangu na wahisani katika harakati za kuwasaidia wahusika kupata karo, vilevile fedha za mahitaji ya kila siku,” aeleza.

Pia, ili kuwezesha wazazi wa watoto hawa kujitegemea, huwaunganisha na taasisi za kutoa mafunzo kupata ujuzi kama vile wa kufuma sweta na kuunda vito na kujipatia pato kuwawezesha kuendelea kushughulikia mahitaji ya wanao

Kufikia sasa watoto saba wanaokumbwa na hali hii wamenufaika kutokana na jitihada zake.

“Watoto watano kutoka kaunti ndogo ya Kinangop na wawili kutoka Kaunti ya Kiambu wamenufaika na wanatarajiwa kujiunga na shule,” aeleza.

Alianzisha kampeni hii baada ya ari yake kuchangiwa na bibi mmoja aliyekuwa akifanya kazi nyumbani kwao.

“Niligundua kuwa mwanamke huyu alikuwa na binti wa miaka 23 aliyeugua ugonjwa huu, suala ambalo lilichangia hata ndoa yake kuvunjika,” aeleza.

Ni hapa aliamua kutafuta njia ya kumsaidia ili kumwezesha bintiye kuendelea na masomo.

“Tayari msichana huyu anatarajiwa kujiunga na shule mwezi Septemba,” asema.

Mbali na hayo, aligundua wazazi wengi walikuwa na mazoea ya kuwaficha watoto wao waliokumbwa na hali hii kutokana na aibu.

Licha ya kwamba jitihada zake hazijatambuliwa, Bi Kimotho ambaye pia ni mhubiri, mfanyabiashara, mkulima na mnasihi wa vijana, anasema kwamba ananuia kuendeleza kampeni hizi katika sehemu zingine nchini.

Ni ndoto anayopanga kuitimiza hasa ikizingatiwa kwamba mwezi Septemba anatarajiwa kujiunga na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kiambu.

“Hapa natarajiwa kusomea ustawi na huduma kwa jamii, kozi ambayo naamini itanipa ujuzi zaidi wa kuimarisha maisha ya watoto hawa na familia zao,” aongeza.