Makala

DAU LA MAISHA: Awika katika nyanja inayochukuliwa kuwa ni ya wanaume

July 13th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HADITHI yake ni ya kutia moyo.

Aliinuka kutoka mhudumu wa mapokezi (receptionist) na kuwa msimamizi wa tawi la kampuni moja nchini.

Hii ni hadithi yake Fransiscah Wanjiru ambaye katika kipindi cha miaka mitano pekee, ameinuka kutoka mhudumu wa mapokezi na kuwa msimamizi wa tawi la Nakuru la kampuni ya Quipbank Trust Limited, kampuni inayohusika na uuzaji na ukodishaji wa magari vilevile vipuri vyake.

Kazi yake hasa inahusisha kushughulikia utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa bidhaa, kuhifadhi, kurekebisha na mauzo ya bidhaa zinazohusiana na magari.

Kwa kawaida yeye hufanya kazi kwa karibu sana na makanika katika kununua vipuri vinavyohitajika.

“Mara nyingi makanika hawa hunishauri kuhusu linalohitajika na baada ya kurekebisha motokaa, ni jukumu langu kulikagua kuhakikisha kwamba liko katika hali nzuri,” asema Fransiscah.

Kwa sasa anasimamia wafanyakazi 33 na pia kushughulikia ugavi na usafirishaji wa bidhaa nchini Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda. Ili kufanya kazi hii vyema, amelazimika kujifunza mambo kibao kuhusu magari na vipuri vyake. Aidha, ana ufahamu kuhusu sehemu zote za magari.

“Kutokana na mlio wa injini, ninaweza kujua tatizo la gari na kipuri kinachohitajika kulitatua,” aongeza.

Kinachofanya hadithi yake kusisimua hata zaidi ni kwamba hana shahada ya digrii huku akisema kwamba mapenzi na bidii yake, vimemwezesha kufika alipo.

“Kama watu wengi nchini ambao safari yao kimasomo haikuwa nyoofu, sikupata fursa ya kujiunga na chuo kikuu baada ya shule ya upili. Baada ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, nililazimika kusomea kompyuta, kisha diploma katika masuala ya mapokezi. Hata hivyo, sikukamilisha diploma hii baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza,” asema mama huyu wa watoto wawili.

Afisa wa maslahi

Alijiunga na shirika hili mwaka wa 2014 kama mhudumu wa mapokezi ambapo mwanzoni alihudumu kama afisa wa maslahi ya wateja.

Hii ilikuwa kutokana na penzi lake katika masuala ya mauzo.

“Nilipojiunga na kampuni hii nilikuwa mhudumu wa mapokezi ambapo pia nilishikilia nafasi hii katika mashirika mengine. Baadaye nilipanda cheo hadi katika idara ya mauzo katika tawi la Nakuru kabla ya kupata wadhifa huu,” aeleza.

Anasema kwamba uzoefu wake katika masuala ya mapokezi umekuwa nguzo kuu katika safari yake kitaaluma.

Aidha, bidii yake imemhakikishia heshima miongoni mwa wafanyakazi wenzake. “Nafurahia kwamba naheshimiwa na wake kwa waume,” aeleza.

Mbali na haya, Bi Wanjiru pia ni mwokaji shupavu, ujuzi aliosomea baada ya kuchochewa na mamake anayemiliki kampuni ndogo ya kutoa huduma za upishi.

Ushauri wake kwa wanawake ni kwamba wanapaswa kuwa tayari kufanya kazi hata ambazo hazitarajiwi kutekelezwa na wanawake.

“Naamini kwamba wanawake wanaweza kufanya kazi bora zaidi wakiajiriwa sababu hujitolea na kujifunza upesi,” asema.