Makala

DAU LA MAISHA: Japo mdogo atumia taji kupiga vita kansa

February 1st, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HUKU ulimwengu ukipanga kuadhimisha siku ya uhamasishaji wa maradhi ya Kansa juma lijalo, utafiti wa Wizara ya Afya unaonyesha kwamba maradhi haya yanazidi kuwa jinamizi kwa wengi hapa nchini.

Hasa kansa ya lango la uzazi imeonekana kuwa tishio kwa maisha ya wanawake wengi ambapo maradhi haya husababisha vifo vya wanawake wanane kila siku nchini Kenya, idadi ambayo ni sawa na vifo 3,286 kila mwaka.

Aidha, kansa hii ndio inaongoza kwa kusababisha vifo miongoni mwa wanaogua maradhi haya, ikilinganishwa na aina zingine za kansa.

Ni takwimu hizi za kutisha ambazo zimemsukuma Sheila Wangeci, mwanamitindo aliyemaliza wa pili katika shindano la urembo la Little Miss World Kenya, Kaunti ya Kirinyaga, kutumia kipaji chake kujihusisha vilivyo katika vita dhidi ya maradhi haya.

Licha ya umri wake mdogo, msichana huyu wa darasa la sita amejizatiti kupigana na maradhi haya. Huduma zake zinajumuisha kuwatembelea wanaogua kansa ambapo katika harakati hizi anaeneza ujumbe wa upendo na matumaini kwao na jamaa zao.

Ni suala lililomsukuma mapema mwaka 2020 kuanzisha mradi wa ‘Cancer Champion Project’.

Pia, amekuwa akikusanya bidhaa za matumizi kama vile nepi za watu wazima kutoka kwa wahisani na kuhakikisha kwamba zinawafikia wanaozihitaji.

Aidha, kampeni hii inahusisha uhamasishaji kuhusiana na maradhi haya na kuhimiza watu kupimwa mapema, ili endapo watapatikana nayo, watatibiwa mapema na hivyo kuokoa maisha.

Mbali na hayo, anaelimisha watu kuhusu maradhi haya, kama mbinu ya kukabiliana na unyanyapaa.

Huku akiendesha shughuli zake katika eneo la Kerugoya, kufikia sasa, ametembelea wagonjwa katika hospitali ya Kerugoya Fortis Medical and Cancer Centre ambapo anapanga ziara zingine sio tu hospitalini, bali pia manyumbani.

“Napanga kukutana na kati ya wagonjwa 10 na 20 kila baada ya miezi miwili,” asema.

Mwito wake ulichochewa na msiba wa kumpoteza nyanyake kutokana na ugonjwa huu.

“Nyanya yangu alifariki kutokana na kansa ya lango la uzazi Oktoba mwaka jana, ambapo nilishuhudia jinsi alivyoteseka,” aeleza.

Aidha, alipata kichocheo baada ya kuhudhuria hafla mbalimbali za kansa ikiwa ni pamoja na Fashion for Cancer, sherehe ambayo ilihudhuriwa pia na waathiriwa wa maradhi haya na wanamitindo.

“Hapa ndipo nilipata mwito wa kuwahudumia waathiriwa kwa kuwaonyesha upendo, kuwashughulikia na kuwapa matumaini,” asema.

Anasema kwamba huduma zake hazijaelekezewa tu wagonjwa, bali jamaa zao na watu wanaowashughulikia. “Mzigo wa maradhi haya kwa kawaida hauathiri tu wanaogua, bali pia jamaa zao ambao husumbuka kuwaona wapendwa wao wakiwa na maumivu, bali na kutaabika kupata pesa za matibabu,” aeleza.

Licha ya ratiba yake kali, masomo yake hayajaathiriwa kwani msichana huyu ameweza kusawazisha vyema kampeni zake na masomo darasani ambayo yameendelea kuimarika.

Kulingana na Wangeci, mradi huu uko katika awamu ya kwanza ambapo ananuia kuhamasisha jamii kuhusika zaidi katika kampeni dhidi ya kansa.

“Naamini kwamba Mungu ananitumia kama chombo cha kuyagusa maisha ya wengi, na hivyo ningependa kuwaomba watu zaidi kuungana nami katika vita hivi,” aongeza.