Makala

DAU LA MAISHA: Nesi wa kwanza nchini kushughulikia saratani

August 24th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

ALIKUWA muuguzi wa kwanza wa nchini kuweka zingatio katika uuguzi wa maradhi ya kansa.

Ana uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu katika nyanja ya uuguzi.

Kutana na Roseline Opindi, muuguzi ambaye amehudumu kwa miaka 35 katika hospitali mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

Aliamua kujitwika mzigo wa kushughulikia wagonjwa wa kansa, wakati ambapo maradhi haya yalikuwa yakihofiwa, na wachache walikuwa tayari kuhudumia walioathirika.

Katika taaluma yake kama mhudumu wa kiafya, ameshughulikia wagonjwa wa kansa kwa takriban miongo miwili.

“Nilihudumu kama muuguzi wa wodi ya wagonjwa wa kansa kati ya mwaka wa 1995 hadi mwaka wa 2014 nilipostaafu katika hospitali ya Kenyatta,” asema.

Ukakamavu na uthabiti wake katika nyanja hii wakati mmoja ulifanya kazi yake kutambuliwa nchini Canada na hata kuwahi hudumu kama naibu msimamizi wa wahudumu katika idara ya onkolojia hospitalini Kenyatta.

“Huo ulikuwa mwaka wa 2006 katika warsha fulani nchini Canada ambapo nilizungumzia maisha ya muuguzi wa kansa nchini Kenya. Kazi yangu ilitawazwa kuwa bora zaidi ambapo niliporejea nchini, nilitambuliwa na bodi ya hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na kupandishwa madaraka,” aongeza.

Kazi yake kama muuguzi ilianza katika miaka ya sabini ambapo alihudumu katika idara tofauti za hospitali mbalimbali ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Machakos na ya kitaifa ya Kenyatta.

Akiwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta alihudumu katika idara ya upasuaji, jinakolojia, na wadi ya kujifungua kabla ya kuhamishwa hadi idara ya rediolojia.

Ni hapa ndipo alikuza nia yake ya kutaka kutaalumika katika huduma ya wagonjwa wa kansa.

“Kwa muda mrefu ni watu wachache pekee waliojua kwamba wahudumu, sawa na madaktari na wataalam wengine wanaohusika katika tiba ya kansa walihitaji mafunzo ya ziada, kwa hivyo nilipowaona wakishiriki katika mafunzo mengi ya ziada, hata mimi nilitaka kuhusika,” aeleza.

Kwa hivyo mwaka wa 1997, pamoja na mhudumu mwenzake wa kiume walipata fursa ya kwenda kusomea zaidi kuhusu matibabu haya nchini Misri kwa ufadhili wa shirika la International Atomic Agency.

“Mafunzo hayo yalihusu kuwahudumia wagonjwa wa kansa ya lango la uzazi,” asema.

Mwaka wa 2000 aidha alishiriki katika mafunzo mengine nchini Scotland.

“Mafunzo haya pia yalihusisha matibabu ya kansa. Hapa, niligundua kwamba kulikuwa na mengi ambayo kama wauguzi hatukuwa tukijua kuhusu matibabu ya kansa, na hivyo mafunzo haya yalinisaidia kuimarisha mwito wangu kama mhudumu,” aeleza.

Hofu

Mwanzoni haikuwa rahisi na hata wakati mmoja alikumbwa na hofu ya kuhudumia wagonjwa hawa.

Alipojiunga na idara hii kwa mara ya kwanza alipelekewa katika wodi ya wagonjwa wa kiume wanaougua kansa ya koo.

“Wagonjwa wengi hapa walikuwa wanawekewa mrija wa kupumua shingoni na kuna wakati ambapo mgonjwa angekohoa na kifaa hiki kuanguka. Ili kuokoa maisha ilikuwa ni lazima ushughulike upesi kwa kukiokota, kukiosha na kukirejesha shingoni mwa mgonjwa, jambo ambalo lilikuwa likiwatia hofu wengi,” asema.

Aidha, anasema kwamba kushuhudia wagonjwa wakilemewa na makali ya uchungu kulimtia hofu, lakini sababu ni mwito, alilazimika kujitia moyo na kuendelea kuwahudumia.

Na ni mwito wa aina hii ambao Bi Opindi ambaye kwa sasa amekuwa akijihusisha katika harakati za ushauri na kutoa mafunzo, anasema unapaswa kukuzwa kwa wahudumu wa kizazi cha sasa.

“Inahuzunisha kwamba siku hizi taaluma hii inachukuliwa tu kama mbinu ya kupata pesa pekee. Kama mhudumu, ili kutimiza kusudi la maisha yako hapa ulimwenguni unapaswa kuwa tayari kujinyima na kuwahudumia wagonjwa bila kuhisi kana kwamba unasumbuliwa,” aongeza.