Makala

DAU LA MAISHA: Usimuone mdogo wa mwili ukamdharau…

September 14th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

AMEKIUKA dhana potovu za kijinsia na kujitosa katika taaluma ambayo kwa wengi, imehifadhiwa wanaume.

Kutana na Cynthia Cherema Mkabane, 25, mhandisi wa masuala ya kieletroniki na kiufundi katika kampuni moja hapa jijini Nairobi.

Kinachofanya hadithi yake kusisimua hata zaidi ndiye mwanamke pekee kati ya wanaume 10 katika idara ya uhandisi ya kampuni hiyo yenye zaidi ya wafanyakazi 200.

Baadhi ya majukumu yake ni pamoja na kuelewa na kutafsiri miongozo ya jinsi ya kutumia mitambo ya kiufundi, kuiunganisha na kutatua matatizo mbalimbali ya kiufundi kwenye mitambo ya kielektroniki.

“Pia, kazi yangu inahusisha kudumisha ubora na usalama wa mazingira ya kufanyia kazi. Hii ni mbali na kuhifadhi na kukarabati mitambo ya kieletroniki, kutafsiri michoro ya kieletroniki, kupendekeza na kutekeleza hatua za kuimarisha mbinu za uzalishaji umeme,’ aeleza.

Kwa kawaida ni kazi inayohitaji sio tu ujuzi wa kiufundi kwani mara kwa mara, anahitajika kutumia nguvu ili kuetekeleza majukumu yake. Hii ni mojawapo ya changamoto ambazo yeye hukabiliana nazo kila siku.

“Hasa mwanzoni changamoto hii ilinilemea kiasi. Nakumbuka mara ya kwanza kuwasili kazini, baadhi ya wafanyakazi wenza walishindwa kuelewa ninavyofanya kazi hii,” asema.

Pia, uwepo wake kwenye idara hii kuliwashtua wenzake wa kike.

“Nakumbuka mara ya kwanza nilipokutana na wafanyakazi wa kike kutoka idara zingine msalani nikiwa nimevalia magwanda yangu ya kikazi, wengi walishangaa na walidhani kwamba sikuwa binti wa kawaida,” aeleza.

Lakini anasema ni taswira aliokumbana nayo hata chuoni, hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa miongoni mwa wanafunzi wachache wa kike waliokuwa wakisomea taaluma hii.

“Nakumbuka tulikuwa wanafunzi sita pekee wa kike kati ya 80 wa kiume. Lakini katika mwaka wangu wa wa nne, tuliongezeka hadi 12 kati ya 112 wa kiume,” aeleza.

Je, alijipataje katika taaluma hii ambayo mabinti wengi huipiga chenga

“Babangu alikuwa akifanya kazi ya uwakala katika kampuni moja ya kusambaza umeme lakini pia alikuwa na ufahamu mpana kuhusu masuala ya uhandisi kwani mara kwa mara aliandamana na wataalamu hawa kazini,” aeleza.

Ni suala lililomfanya Bi Mkabane kujawa na kiu ya kutaka kujua mengi kuhusu kazi hii.

“Mbali na hayo, tangu zamani nilifurahia sana kupata suluhu la kila tatizo nililokumbana nalo na uhandisi unanipa fursa hii,” asema.

Kwa hivyo alipopata alama nzuri katika shule ya upili na kuwekwa kwenye kozi hii, hakuhisi kana kwamba kapotea.

Lakini haikuwa rahisi.

“Mwanzoni, wazazi wangu na hasa mama yangu alikuwa na wasiwasi tele kuhusu iwapo nitatoboa, lakini muda ulivyoendelea kusonga, imani yake iliimarika na hata akaanza kunishabikia,” asema.

Aidha, anasema kwamba kama mhandisi wa kike, amelazimika kutupilia mbali baadhi ya mitindo ya kike.

“Kwa mfano, kazi hii inamhitaji mhusika kuwa mtulivu kabisa kumaanisha kwamba hata mavazi lazima yawe yatakayokusaidia kufanya kazi bila tatizo. Kwa hivyo, kila siku utanipata nimevalia jinzi, tishati na viatu vya raba. Aidha, nywele zangu ni za kiasili, mtindo ambao hautanihitaji kuzishughulikia kila mara. Pia, vipodozi kidogo vimenipa chenga kwani sina muda wa kujirembesha kila mara,” aeleza.

Lakini hayo yote hayamkoseshi raha. “Dhana kwamba mwanamke sio kamili ikiwa hajajipodoa au kuvalia marinda na viatu vya visigino virefu, imewanyima wanawake wengi fursa ya kujihusisha na baadhi ya taaluma wanazofurahia,” aongeza

Anawashauri wasichana kupuuza vizingiti hasa vinavyohusishwa na jinsia ambazo zinawazuia kutimiza ndoto zao kitaaluma.