Mwanaharakati mashuhuri David Kimengere arejea nchini baada ya miaka 3 uhamishoni

Mwanaharakati mashuhuri David Kimengere arejea nchini baada ya miaka 3 uhamishoni

Na BENSON MATHEKA

MWANAHARAKATI mashuhuri David Kimengere Waititu maarufu kama Sauti ya Wanyonge, amerejea nchini baada ya kuishi uhamishoni Ulaya kwa miaka mitatu.

Bw Kimengere aliyekuwa akiishi Iceland, aliwasili Nairobi Jumamosi saa tatu na nusu asubuhi akisindikizwa na maafisa wa usalama wa Iceland kwa kile alitaja kama kuhakikishiwa usalama wake safarini.

Mwanaharakati huyo alitoroka Kenya 2018 akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kwa kutishwa na watu wenye ushawishi ambao hawakufurahishwa na juhudi zake za kutetea masikini.

“Nimefurahi kurejea Kenya baada ya miaka mitatu. Ninataka serikali ya Kenya kunihakikishia usalama wangu. Sitachoka kutetea wanyonge wa nchi hii na ulimwengu kwa jumula kwa sababu huo ndio wito wangu,” alisema Bw Kimengere ambaye ni katibu mratibu wa chama cha Commonwealth Voters Right s and Privileges Association (COWEVOPRA).

Mwanaharakati huyo alisema kwamba wakati huu ambao Kenya inaelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao, atahamasisha wapigakura kura haki zao ili wafanye uamuzi huru na wa haki.

“Nchi hii itajengwa na wanyonge lakini ni lazima wafahamu haki zao kwanza. Kazi yangu kabla ya uchaguzi huo itakuwa ni kuhakikisha wanafahamu haki zao ili waweze kufanya uamuzi huru na wa haki,” alisema Kimengere, mzaliwa wa Othaya kaunti ya Nyeri.

Alielezea azima yake ya kugombea kiti cha ubunge cha Othaya ambacho aliwania kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

“Nimerejea nchini wakati wa siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na watu wa Othaya wameniomba nifikirie kuwa mwakilishi wao bungeni. Itakuwa fursa nzuri ya wanyonge wa nchi hii kupata mwakilishi wao katika Bunge la Kitaifa,” akasema Bw Kimengere.

Alisisitiza kuwa Kenya inahitaji uongozi unaojali maslahi ya masikini na sio mabwanyenye wanaotoka familia za waliokuwa watawala.

“Tutabadilisha siasa za nchi yetu. Tuko na kazi kama wanyonge na tutaifanya bila woga hata tukitishwa,” alisema.

Bw Kimengere alishukuru serikali za Norway na Iceland kwa kumpa hifadhi kwa miaka mitatu.

You can share this post!

TAHARIRI: Mazimwi yanayokula soka yetu yazimwe

Macho kwa Kamworor akivizia rekodi ya dunia ya Eliud...

T L