Habari Mseto

David Major apelekwa hospitalini

November 19th, 2020 2 min read

Na WANGU KANURI

ALIYEKUWA msanii, mwanamuziki na mpiganiaji wa tuzo ya shindano la Tusker Project Fame, David Ogola almaarufu David Major, amepelekwa hospitalini wahudumu wamshughulikie aondokane na uraibu wa dawa za kulevya.

Hii ni baada ya picha zake kuonekana katika mitandao ya kijamii akionekana mwenye uchafu na udhaifu mwingi wa mwili. David Major alionekana katika barabara ya Mirema kule Roysambu na msamaria mwema, Tony Ingosi almaarufu Shobol, ambaye alimkaribisha nyumbani mwake na kumpa chakula.

Aidha David Major hakutaka kulala kwake Shobol huku akimweleza kuwa angependa kulala katika klabu moja eneoni.

Mchekeshaji mwenye umaarufu sana Alan Love, ambaye anavuma katika mtandao wa kijamii wa Tiktok, alijihusisha katika kumtafuta David Major huku akijitolea kuhakikisha kuwa David Major amegeuza hali yake ya maisha.

Akiandika katika ukurasa wake wa Facebook mnamo Novemba 17, 2020, Alan Love aliwauliza wafuasi wake kama kuna mtu anayejua kule David Major aliko kwani alikuwa akiendesha gari lake kule Kasarani akimtafuta, juhudi ambazo zilionekana kugonga mwamba.

“Kuna mtu anayejua kule ninaweza mpata David Major? Ninaendesha gari huku Kasarani nikimtafuta,” akaandika Alan Love.

Baada ya saa chache, Alan Love aliwaambia wafuasi wake kuwa alimpata David Major huku akimshukuru mwanamke mmoja kwa jina Margaret kwa kumchukua Major, kumpa pahali pa kuogea, kumpa mavazi mapya na kuisuka nywele yake. Alichukua picha ya wawili hao na kuiweka katika ukurasa wake wa Facebook. Isitoshe, akawarai wakenya kumsaidia David Major kwa chochote wangeweza.

Hali kadhalika, Alan Love alieleza kuwa kuna mambo mengi ambayo yalimfanya David Major kuishia hapo alipo huku akiwaomba wakenya wasiwe na haraka ya kusema mambo ambayo hawajui ukweli wake. Ukweli ni kwamba, David Major alitumia dawa za kulevya huku akiishia kuwa mdhaifu wa afya, kama alivyodhibitisha Alan Love.

Isitoshe, Alan Love aliwakumbusha wakenya kuwa maisha ni panda shuka; leo uko juu kesho yake uko chini hivi hakuna haja kumhukumu mwenzako akiwa chini. Alikuwa na haya ya kusema:

“Watu wana mengi ya kusema kuhusu wengine wakati ambapo mtu ako chini. Swali linalobaki kinywani mwangu ni hili: Je watu hao walio chini wanapaswa kupatiwa nafasi nyingine ama hawafai kwa sababu walikifanya hiki ama kile?”

Itakumbukwa kuwa Alan Love alipitia tukio kama hili mapema mwaka huu baada ya Covid-19 kubisha nchini huku nyumba aliyokuwa amekodisha ikifungwa na mwenye nyumba huku ikimlazimu kuondokea mitaani.

Isitoshe, kama alivyosimulia, hakuna rafiki hata mmoja aliyejitolea kumuokoa alipokuwa amefungiwa nyumba huku ikimlazimu kulala katika nyumba ya mlinda lango mmoja ambaye alimuonea huruma. Alan Love alieleza kilichomfika kwa kuchukua video na kuiweka katika mtandao wa kijamii huku akiwarai Wakenya wamuonee huruma na kumsaidia. Wakenya walishirikiana na kumchangia hadi wakati ambapo alirejea katika hali yake ya kawaida.

Mkondo uu huu, ndio ulielekezewa David Major, huku Alan Love akiweka nambari ya Paybill ya kumsaidia Major katika ukurasa wake wa Facebook. Wakenya waliombwa wajitokeze kwa wingi na kumsaidia David Major kurejea hali yake ya kawaida kabla hajawa mlanguzi wa dawa za kulevya. Kabla ya maisha kuchukua mkondo tofauti, David Major alikuwa akifanya kazi kama mhandisi wa sauti nchini Kenya.

Mamake David Major ni marehemu daktari Margaret Ogola, mwandishi tajika wa vitabu na daktari. Mwendazake daktari Margaret Ogola alifahamika sana nchini Kenya wakati kitabu chake The River and the Source kilitahiniwa katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, kabla hajafa kwa kansa mnamo 2011.