Michezo

David Silva ayoyomea Sociedad

August 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO wa zamani wa Manchester City, David Silva, ameingia katika sajili rasmi ya Real Sociedad ambao wamejinasia huduma zake kwa mkataba wa miaka miwili.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 34 alitamatisha kipindi cha miaka 10 cha kuvalia jezi za Man-City mnamo Agosti 15, 2020 katika mechi iliyowashuhudia waajiri waliokuwa waajiri wake wakibanduliwa na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Lisbon, Ureno.

Silva ambaye alisajiliwa na Man-City kutoka Valencia mnamo 2010, aliwajibishwa uwanjani Etihad katika jumla ya mechi 436 na akasaidia kikosi hicho kunyanyua jumla ya mataji 14.

Silva anaingia katika sajili rasmi ya Sociedad baada ya kukataa ofa ya Lazio kutoka Italia ambao walikuwa radhi kumpokeza mkataba wa miaka mitatu.

Sociedad walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu katika nafasi ya sita jedwalini na walijipata katika ulazima wa kutafuta mwanasoka kizibo cha Martin Odegaard aliyerejea Real Madrid baada ya kipindi chake cha mkopo kambini mwao kutamatika.

Akivalia jezi za Man-City, Silva aliwajibishwa katika mechi 309 za EPL ambapo alifunga mabao 60 na akachangia pakubwa mafanikio ya kikosi hicho kutwaa mataji manne ya EPL mnamo 2012, 2014, 2018 na 2019.

Katika mechi nyinginezo zisizokuwa za EPL na UEFA, alichezeshwa na Man-City mara 57 na akasaidia kikosi hicho kutwaa makombe mawili ya FA, matano ya League Cup na matatu ya Community Shield.

Silva anashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka anayejivunia kusakatia Man-City idadi kubwa zaidi ya mechi (70) kwenye UEFA chini ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Uhispania kilichonyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2010 na mataji ya Euro mnamo 2008 na 2012. Msimu mpya wa 2020-21 katika La Liga umeratibiwa kuanza Septemba 12, 2020.