Habari MsetoSiasa

Dawa ya kuzima Ruto kuingia Ikulu 2022 ni BBI – Atwoli

March 10th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MPANGO wa Maridhiano (BBI) utatumika kuhakikisha Naibu Rais William Ruto hapati tiketi ya kuwania urais 2022, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi (COTU) Francis Atwoli alifichua Jumatatu.

Bw Atwoli alidokeza kwamba BBI itatumiwa kuimarisha Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili ya viongozi, na hatua hiyo itafanya iwe vigumu kwa Dkt Ruto kuruhusiwa kuwania urais.

“Jina lake Ruto halitakuwa kwenye karatasi ya kura kwa sababu ya maadili yake. Tukitumia Sura ya Sita ya katiba kikamilifu au tuiimarishe katika BBI, vyama vitaruhusiwa kuteua wagombeaji wenye maadili bora pekee,” akasema Bw Atwoli akiwa Kisumu.

Nacho chama cha ODM kupitia kwa Katibu Mkuu Edwin Sifuna, kilidai kuwa Dkt Ruto amezingirwa na viongozi ambao wanafanya mienendo yake itiliwe shaka.

Alisema haya akirejelea sakata ya utapeli wa zabuni ya vifaa vya kijeshi inayomshusisha aliyekuwa waziri Rashid Echesa.

Bw Sifuna alisema ODM kitaunda serikali ijayo ifikapo 2022, na kupuuzilia mbali azimio la Dkt Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Misimamo hiyo imetokea wakati ambapo Dkt Ruto anazidi kulalamika kwamba kuna njama zinazokusudia kuvuruga azimio lake kuongoza Wakenya.

Bw Sifuna alikosoa msimamo wa Dkt Ruto kwamba njia pekee ya maadui wake kumzuia kuingia ikulu ni kumuua.

“Sisi hatumwombei mabaya. Hatumpangii hila zozote. Tunataka awepo wakati huo ili aone jinsi serikali ya ODM itaendesha nchi ambayo haina ukabila wala chuki kuanzia 2022,” akasema katika mahojiano redioni.

Wikendi iliyopita, Seneta wa Siaya James Orengo alifichua mipango ya kumng’oa mamlakani Dkt Ruto.

Awali, aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee David Murathe alisisitiza haitawezekana Rais Kenyatta kumkabidhi Dkt Ruto mamlaka atakapoondoka uongozini.

Dkt Ruto na wandani wake katika kikundi cha Tangatanga humkashifu Bw Odinga kwa kutumia handisheki kupata mwanya wa kuingia serikalini.

Misimamo mikali ya viongozi wa mrengo huo inaaminika kusababisha mkutano wa kuhamasisha umma kuhusu BBI ufutiliwe mbali katika Kaunti ya Uasin Gishu ambayo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto.

Mkutano wa BBI eneo la Rift Valley sasa umepangwa kuandaliwa mjini Nakuru wiki ijayo.