Afya na Jamii

Dawa za kusaidia kupata ashiki haziathiri akili, Watafiti sasa wabaini

February 12th, 2024 1 min read

Na CECIL ODONGO

DAWA ambazo zinatumika kutibu ubutu wa hisia za mapenzi kwa wanaume haziwezi kusababisha maradhi ya kiakili (Alzheimer), Watafiti wamebaini.

Kumekuwa na dhana kuwa dawa hizo zikitumika, zinaweza kusababisha mtu apotoke kiakili baada ya kufika kiwango fulani cha matumiz. Hii ni kwa sababu kwa kiasi fulani zinaweza kuathiri uwajibikaji wa seli za ubongo.

Hali hii imekuwa ikiwafanya wengi kuingiwa na wasiwasi kuwa watakuwa wehu licha ya dawa hizo kuwasaidia kupata ashiki na kuwaepushia aibu.

Hata hivyo, watafiti wa Shule ya Famasia (UCL) Uingereza wamegundua kuwa hakuna hatari zozote za kutumia dawa hizo mradi kanuni zote zifuatwe.

Nyingi za dawa za kuamsha hisia za mapenzi zinazotumika kwa wanaume, mwanzo zilikuwa zikitumika katika matibabu ya shinikizo la damu.

Dawa hizo zinasaidia katika kupanua mishipa ya damu kwenye uume na kusababisha iwe rahisi kupata ashiki wakati wa tendo la ndoa.

Baada ya kupanuka kwa mishipa hiyo, huwasiliana na ubongo na kusababisha iwe rahisi úume kuamka kabla na wakati wa tendo la ndoa.

Kuafikia msimamo huu, watafiti hao walihusisha wanaume ambao wamekuwa wakitumia dawa hizo za kuongeza ashiki. Baada ya muda fulani kuwapitisha kwenye uchunguzi wa kimatibabu wa kuona iwapo walikuwa wameathirika, ilibainika wengi wao bado walikuwa sawa.

“Hatuwezi kusema kabisa kuwa dawa za kuchangia mtu kusisimka wakati wa mapenzi hazina athari au huvuruga akili ila matokeo haya yanadhihirisha kuwa hakuna hatari zozote,” akasema.

Watafiti hao hata hivyo, walifichua kua wamepiga hatua kubwa katika kusaka matibabu kwa maradhi ya kiakili hasa kwa wale ambao ndiyo maradhi hayo yanaanza.

Walisisitiza wanahitaji kuwa na dawa ya kutibu maradhi hayo au kuyapunguza kwa kuwa ni hatari na yanaweza kusababisha mauti.