Dawa za kutibu akili taahira zinapogeuzwa ulevi wa mauti

Dawa za kutibu akili taahira zinapogeuzwa ulevi wa mauti

Na MWANGI MUIRURI

Kwa muda mrefu sasa, biashara ya mihadarati ambayo imezua visa vya ujambazi wa kikatili miongoni mwa vijana katika jamii imekuwa ni ile ya kushirikishwa katika usiri wa vichochoro na vichaka lakini sasa imehamia katika maduka rasmi yaliyo na leseni na ikishirikishwa na wataalamu wa kimatibabu.

Idara za kiusalama nchini sasa zimekiri kwamba zinatatizika na hali hii mpya ambapo hilo duka lililo karibu nawe na ambalo hukuuzia dawa halali ya kimatibabu huenda ndilo kwa sasa linaharibu kesho ya vijana wa mtaa wa kwenu kupitia kuwauzia dawa zinazotumika kutibu na kutuliza makali ya akili taahira.

Dawa hizo ambazo huorodheshwa kama benzodiazepines yakitumiwa na wasio na matatizo ya kiafya na kisha yachanganywe na ama bangi, miraa au pombe, huishia kuwa mihadarati hatari ambayo huzua ulevi wa kushinikiza utekelezaji mauti.

Maafa

Utumizi wa dawa hizo sasa unahusishwa na kupanda kwa visa vya kikatili ambapo vijana wanaua kiholela, hutekeleza ghasia katika jamii na kuamua kujiua kwa wingi huku hata wanafunzi wanaozitumia wakiorodheshwa kama wanaoongoza ujambazi wa kuchoma mabweni na madarasa shuleni.

Pia, walio katika sekta za uchukuzi, wakishatumia dawa hizo ndio wengi wanaishia kuzua ajali za bodaboda na magari na pia kuua abiria kupitia kuwarusha nje ya magari yaliyo katika mwendo wa kasi.

Licha ya kwamba madawa haya yanafaa tu kuafikiwa na wagonjwa halali wa matatizo ya kiakili, na wawe na cheti rasmi kilichotiwa sahihi na daktari wa matatizo hayo, vijana hawa huwa wabunifu kiasi kwamba huishia kuyapata kwa hila.

Baadhi ya mbinu ambazo hutumika ni kuiba dawa hizo kutoka kwa waathiriwa, kughushi vyeti na kujiangazia kama walio na matatizo ya kiakili, kusaka huduma za madaktari wafisadi ambao huwapa vyeti hivyo na pia wahudumu na wamiliki wa maduka ya madawa wakiongozwa na ukora wa kuunda faida kuwauzia kisiri.

Mtaani, dawa hizo hufahamika kama tap taps, Kuruga, Kuruka, Matembe, Kokoto, D5 na kadhalika kulingana na lugha inayotumika katika maeneo mbalimbali nchini.

Shida ni kwamba, dawa hizi licha ya madhara hayo makuu huwa ya bei rahisi na hupatikana kwa urahisi na kuna wengi ambao wamezikumbatia kama biashara ya faida ambapo wakishanunua tembe hizo kwa senti tu kwa kila moja, huishia kuuza kwa Sh5 kwa kila moja na kuunda faida za kuvutia.

Ukinunua kwa bei ya ujumla, tembe 3, 000 huuzwa kwa Sh1, 000 na kisha kuuzwa kwa Sh5 kila moja yake hivyo basi kuvuna Sh15, 000 ambapo faida ni Sh14, 000. Kutokana na utumizi wa juu, kunao ambao kwa siku huripotiwa kujipa zaidi ya Sh140, 000 kwa siku kama faida haswa katika miji mikuu kama Nairobi, Mombasa, Nakuru na Kisumu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Huduma za Kimatibabu katika Hospitali Kuu ya Murang’a Dkt Leonald Gikera dawa hizi za kutibu akili taahira zikitumiwa na wasioathirika huzua “hali ya msisimko hatari wa kuzua ghasia, hupandisha mvuto wa kutekeleza yasiyo ya kawaida na hatimaye hulemaza na huua.”

Anasema kuwa ni madawa hatari ambayo pia hutwika wanaozitumia vibaya kupooza kwa viungo, mipigo ya damu kupindukia, kulemewa kwa moyo kukithi msukumo kupindukia wa damu na pia huharibu viungo muhimu kama maini na figo.

Dkt Gikera anasema kuwa licha ya kwamba kuna aina 2, 000 za dawa hizo sokoni katika safu ya Ulimwengu, hapa nchini kuna aina 10 ambayo hutumika.

Mshirikishi wa masuala ya kiusalama Ukanda wa Kati Bw Wilfred Nyagwanga aliambia Taifa Leo kwamba jamii za eneo hilo zimeathirika pakubwa na utumizi wa dawa hizo “kiasi kwamba nimeunda kamati maalum ikiwa na kikosi maalum pia kukabiliana na changamoto hii.”

Aliwataka viongozi wa eneo hilo katika mabunge ya kitaifa na ya Kaunti wawajibikie suala hilo na waunde sheria mwafaka za kuzima ukora unaopenyezwa katika dawa hizo halali.

Bw Nyagwanga anasema kuwa ripoti za ujasusi kuhusu kero la madawa haya zimetambua Ecstasy, MDMA, Rohypnol, D5, GHB na Ketamine kama yanayotumiwa vibaya eneo hilo.

Bi Catherine Wambui ambaye ni mama mzazi wa vijana watatu wa kiume katika mji wa Maragua Kaunti ya Murang’a anasema kuwa hivi majuzi alipigwa na mmoja wao aliye na umri wa miaka 17.

“Licha ya kwamba kijana huyu alifaa kufanya mtihani wake wa Darasa la nane (KCPE) Machi iliyopita katika shule ya msingi ya Mugumo-ini iliyo katika tarafa ya Ichagaki, hakuufanya kwa kuwa amezama katika utumizi wa madawa haya,” asema.

Mwingine aliye na miaka 21 kwa sasa alifaa kufanya mtihani wake wa Kidato cha Nne (KCSE) miaka mitatu iliyopita “lakini kwa sasa ako katika kidato cha pili kwa kuwa amekuwa akitumia dawa hizo na kuishia hata kulazwa hospitalini. Ni watoto ambao kwa sasa hata huwa wanatishia kuninajisi.”

Anasema kuwa dawa hizo hununuliwa kutoka maduka “yanayofahamika vyema na pia kuuzwa mtaani na wanaojulikana vyema.”

Anasema kuwa wakati vijana hao wake hawajatumia dawa hizo, “huwa wanakiri ni wapi huuziwa na huwa ninapasha maafisa wa kiusalama habari hizo lakini hakuna afueni nimepata.”

Maadili

Mwenyekiti wa Maendeleo ya wanawake Mlima Kenya Bi Lucy Nyambura anasema kuwa “shida kubwa tuliyo nayo kwa sasa ni dawa hizi kuwa na bei rahisi, ukosefu wa maadili kwa walio na maduka ya mauzo ya madawa, baadhi ya wahudumu hospitalini kuyaiba kutoka stoo na kuzindua biashara haramu ya kuyauzia vijana mitaani huku serikali ikijua bila kufanya kitu.”

Bi Nyambura anasema kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, muungano wake umepokea zaidi ya visa 12, 000 vya watoto kugeuka kuwa hatari kwa familia zao na jamii kwa ujumla kutokana na utumizi wa dawa hizo.

Mshirikishi wa masuala ya kiusalama Rift Valley Bw George Natembeya anafichua kuwa madawa haya na matumizi yake mabaya katika jamii ni suala ambalo limekuwa likijadiliwa katika ngazi za juu za wizara ya Usalama wa Ndani na kutolewa kwa mwongozo kwamba yakabilianwe nayo.

“Lakini shida ni kwamba, maduka haya yanathibitiwa na mamlaka ya kusimamia taaluma na biashara ya madawa. Pia, ni vigumu sana kumnasa muuzaji aliye na duka lake ikiwa ametumia cheti cha kupendekezwa mgonjwa atumie dawa hizo. Ni suala ambalo linahitaji uchunguzi wa kina na ulio na ubunifu na jamii ijitolee kutoa walalamishi na mashahidi,” asema.

Alisema kwamba dawa hizo yanatumika na watengenezaji wa pombe haramu ili kuzipa makali yanayotamaniwa na walevi wa kiwango cha chini ambao haja yao ni kulewa kwa gharama ya chini zaidi iwezekanavy.

“Utapata kijana ameingia kwa kichochoro akiwa sawa na akijinunulia glasi moja ya Sh10 ya pombe haramu iliyochanganywa na dawa hizo, anageuka kuwa shetani aliye na msukumo wa kutekeleza hata mauaji. Ni hatari ambayo ni lazima ikabilianwe nayo,” asema.

Mbunge wa Nandi Hills Bw Alfred Keter kwa sasa ameandaa Mswada bungeni akitaka maduka ya kuuza dawa mitaani yazimwe ruhusa ya kuuzia wateja ambao hawana cheti rasmi kilichotiwa sahihi na mkurugenzi wa kimatibabu wa eneo ili kuzima visa vya vyeti hivyo kuundwa kiharamu.

Kwa yeyote atakaneyanswa akikiuka sheria hiyo ikiwa itatimia, Bw Keter amependekeza mshukiwa awe akitozwa faini isiyopungua Sh30, 000 au kifungo gerezani kisichozidi miaka mitatu au zote mbili ikiwa atahukumiwa kuwa kwa hatia.

You can share this post!

Viongozi wasifu wakazi wa Garissa kwa urithi wa Haji

KIKOLEZO: Waliambiwa ‘mtaachana tu’!