Habari

DCI alaumu ufisadi kwa ongezeko la kansa nchini

July 30th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

WAFANYABIASHARA matapeli wanaouza bidhaa ghushi, hasa vyakula, wamelaumiwa kwa ongezeko la maradhi ya kansa yanayosababisha maelfu ya maafa kwa Wakenya kila mwaka.

Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) Jumanne ilisema kunahitajika kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya taasisi zinazotegemewa kukabiliana na uhalifu nchini ili kukomesha matapeli hao.

Akizungumza jana jijini Nairobi wakati wa kongamano la Wakurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Wakurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu kutoka Afrika Mashariki, Mkurugenzi wa DCI, Bw George Kinoti alisema ni muhimu polisi, waendeshaji mashtaka na majaji kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa wafanyabiashara wanaohatarisha maisha.

“Bidhaa zilizopitwa na muda wa ubora zinaingizwa nchini na kupakiwa kama bidhaa mpya ilhali ziliharibika zamani. Ni ulafi kwa kiwanda kupakia vitu ambavyo wanajua vitadhuru watu,” akasema Bw Kinoti.

Alisema hayo siku moja baada ya Gavana wa Bomet, Dkt Joyce Laboso kufariki kwa saratani, siku chache baada ya Mbunge wa Kibra, Bw Ken Okoth pia kufa kwa kansa.

Ripoti ya shirika la International Agency for Research on Cancer iliyotolewa mapema mwaka huu, ilionyesha maambukizi mapya kila mwaka nchini huwa ni 47,887, na Wakenya wasiopungua 32,987 hufariki kila mwaka kwa kansa.

Bw Kinoti alifichua kwamba kando na bidhaa zilizooza ambazo hupakiwa upya na kuuzwa nchini, nyingine hupakiwa katika nchi jirani na kuletwa Kenya kama zinazostahili kuliwa na binadamu.

“Tunasema kuna ongezeko la ugonjwa huu na ule, ilhali tunajiangamiza wenyewe. Sote sasa tuseme imetosha. Kuendelea mbele, inafaa tusihurumie watu hawa walafi ndipo tuwakomeshe,” akasema.

Vyakula vilivyojaa sumu kama vile sukari, mchele, nyama, mafuta ya kupika na hata vinywaji kama vile pombe vimekuwa vikinaswa nchini mara kwa mara. Baadhi ya mbinu za kilimo, ufugaji na uhifadhi wa vyakula pia huchangia kuwepo kwa vyakula vya sumu sokoni.

Lakini hakujaonekana hatua kali zikichukuliwa dhidi ya wahusika wanaonaswa katika biashara hizo haramu zinazoangamiza taifa.

Mbali na usafirishaji wa bidhaa ghushi kati ya mataifa ya ukanda huu, changamoto nyingine sugu ni kama vile ulanguzi wa binadamu, ugaidi, ulanguzi wa dawa za kulevya na utapeli wa kuhalalisha pesa haramu.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji alisema ushirikiano kati ya afisi yake na DCI umeleta mafanikio katika kupambana na uhalifu, na mwenendo huo unafaa kukumbatiwa kati ya mataifa ya Afrika Mashariki.