Habari Mseto

DCI azimwa kumchunguza Prof Ojienda

December 31st, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JUHUDI za mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji kumshtaki wakili Profesa Tom Ojienda kwa ufisadi wa Sh89 milioni ziligonga mwamba mahakama kuu iliposambaratisha hatua hiyo.

Jaji Enoch Chacha Mwita aliwazuia DPP na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) George Kinoti kumchunguza na kumfungulia mashtaka Prof Ojienda ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu kutoka kwa kiwanda cha kutengeneza sukari cha Mumias (MSC).

Prof Ojienda alifika mahakamani mwendo was aa nne asubuhi baada ya kuzuiliwa kwa siku tatu katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Alipoachiliwa Jumapili usiku aliamriwa afike kortini Jumatatu saa nne kujibu mashtaka.

Lakini DPP na DCI walizimwa na mahakama kuu kumshtaki mlalamishi huyo aliyewashtaki katika mahakama kuu.

DCI alizimwa akiendelea kumchunguza Prof Ojienda kwa kazi alizofanyia MSC hadi kesi aliyowasilisha isikizwe na kuamuliwa.

Seneta James Orengo alipomtetea wakili Prof Tom Ojienda Desemba 31, 2018. Picha/ Richard Munguti

Jaji Mwita alisema DPP aliwasilisha rufaa kupinga maagizo ya Jaji Isaac Lenaola ya 2016 alipozima hatua za tume ya kuchunguza ufisadi nchini (EACC) kumchunguza na kumfungulia mashtaka Prof Ojienda kwa ajili ya ada aliyolipwa kwa kuwakilisha MSC mahakamani.

Jaji Mwita aliombwa na mawakili zaidi ya 30 waliomwakilisha Prof Ojienda azime hatua ya DPP ya kuwashika washukiwa Ijumaa na kuwazuilia kwenye korokoro za polisi.

“Baada ya kupokea mawasilishi ya mawakili na kusoma ushahidi  wa mlalamishi na kusoma taarifa iliyowasilishwa mbele yangu ni wazi kesi hii inaendelea katika Mahakama ya Rufaa,” alisema Jaji Mwita.

Jaji huyo alisema itakuwa ni ukandamizaji wa hali ya juu wa haki za Prof Ojienda ikiwa DPP ataruhusiwa kumfungulia Prof Ojienda kesi ilhali kesi iliyosawa hii inaendelea kusikizwa katika mahakama  ya rufaa.

Jaji huyo alisema mwenye kuwasilisha kesi dhidi ya Prof Ojienda katika mahakama ya rufaa sio mwingine ila ni DPP.

Prof Ojienda anakabiliwa na mashtaka sita ya kupokea zaidi ya Sh11milioni kwa njia ya undanganyifu kutoka kwa MSC akidai alikitetea kiwanda hicho katika kesi zilizoshtakiwa mahakama mbali mbali kati ya 2012-2018.

Kiongozi wa mashtaka Alexander Muteti aliyemwakilisha DPP akiwa kortini Jumatatu. Picha/ Richard Munguti

Mahakama na mawakili 30 waliomwakilisha  Prof Ojienda wakiongozwa na Mabw Okong’o Omogen, Danstan Omari, James Orengo , Dkt Otiende Amolo na Dkt John Khaminwa  polisi wanaochunguza kesi dhidi ya mlalamishiwalifahamishwa hayo n ahata kupewa ushahidi lakini wakaupuuza.

“Hakuna shtaka la uhalifu itafunguliwa dhidi ya wakili yeyote yule kutokana na kazi anayotekeleza kila siku,” Dkt Amolo alimweleza Jaji Mwita.

Aliongeza kusema ikiwa mteja hajaridhishwa na ada aliyolipishwa na wakili Mahakama kuu ipo awasilishe madai lakini sio “polisi kumwandama.”

Jaji Mwita alisitisha hatua ya kumshtaki Prof Ojienda na kuamuru kesi hiyo itajwe Feburuari 18 mwaka huu.

Jaji Mwita aliamuru DPP na DCI waliotajwa kama washtakiwa na Prof Ojienda

Awali kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Muteti alikuwa amewasilisha kesi dhidi ya Prof Ojienda mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Bi Mutuku aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18 kusubiri uamuzi kutoka mahakama kuu.