Habari Mseto

DCI kumhoji Washiali kuhusu uvamizi videoni

February 14th, 2020 1 min read

Na BENSON AMADALA

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inamchunguza Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali kuhusu madai kuwa alimdhulumu mwanamume mmoja aliyeshukiwa kufyonza mafuta kutoka kwa trekta moja miaka mitatu iliyopita.

Bw Washiale ambaye ni kiranja wa wengi bungeni, anatuhumiwa kumdhulumu mwanamume huyo asiyetambuliwa mnamo 2015.

Hii ni baada ya video moja kuchipuza mitandaoni mwezi jana ikimwonyesha mbunge huyo akimpiga teke na kumzaba kofi mwanamume huyu, akimkemea kwa kufyonza mafuta kutoka kwa trekta ya kusafirisha miwa.

Lakini Bw Washiali alisema wale ambao wanasambaza video hiyo wanalenga kumhujumu kisiasa.

Afisa wa DCI ukanda wa Magharibi Bw Shem Nyamboki, alisema Alhamisi kwamba polisi wameandikisha taarifa kutoka kwa mwanamume huyo na kuthibitisha kuwa aliripoti kisa hicho kwa kituo kimoja cha polisi Mumias lakini hatua haikuchukuliwa.

Bw Nyamboki akasema: “Sasa tunachunguza suala hilo na tumepiga hatua kwani sasa tunalenga kumhoji mbunge huyo na kuchukua hatua zifaazo.”

Polisi wamepata rekodi matibabu na zinazoonyesha kuwa mwanamume huyo alitibiwa baada ya kushambuliwa karibu na shamba la miwa.

Katika video hiyo, mbunge huyo anasikika akimkemea mwanamume huyo kwa kufyonza mafuta kutoka kwa trekta hiyo inayotumiwa kusafirisha miwa hadi kituo cha kampuni ya sukari ya Mumias.

Video hiyo iliibua kero kuu katika mitandao ya kijamii huku wakazi wakipendekeza kuwa Bw Washiali akamatwe na kushtakiwa.