DCI waahidi Sh10m kwa atakayenasa mshirika wa magaidi

DCI waahidi Sh10m kwa atakayenasa mshirika wa magaidi

Na BRIAN OCHARO

IDARA ya polisi sasa imejitenga na utekaji nyara wa mhukumiwa wa ugaidi aliyekamilisha kifungo chake, Elgiva Bwire Oliacha, na kumtaja kama mtu hatari anayetishia usalama wa nchi.

Bwire alitoweka baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana alipokuwa akiondoka mahakamani wiki iliyopita. Wakili wake, Prof Hassan Nandwa, pia alitoweka kwa njia zisizoeleweka lakini akapatikana Mwingi Jumatatu. Prof Nandwa ameshindwa kuzungumzia masaibu yake tangu alipopatikana.

Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) jana ilimworodhesha Bwire miongoni mwa washukiwa wengine wa ugaidi, na kusema yeyote atakayesaidia kupatikana kwake atalipwa zawadi ya Sh10 milioni. Washukiwa wengine ambao wanatakikana kwa kupanga mashumbilizi ni Barigi Abdikadir Haila kutoka Moyale, Trevor Ndwiga kutoka Nairobi, Muhamad Abubakar kutoka Mombasa na Salim Rashid ambaye anaaminika kuwa nchini Mozambique kwa wapiganaji wa ISIS.

Kulingana na DCI, inaaminika Bwire ameenda mafichoni kupanga mashambulio ya kigaidi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. ‘Huduma ya Polisi ya Kitaifa inafahamisha umma kwamba, ana silaha hatari na inaomba taarifa zozote kuhusu aliko,” taarifa hiyo ikasema.

Hayo yalijiri huku ikifichuka kuwa, maafisa wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) wamewakamata washukiwa wengine wawili ambao wanadaiwa walikuwa wanaelekea Somalia kujiunga na Al-Shabaab.

Bw Rajabu Mwinyihamisi Hamza na Iqram Ramadhan Rashid walikamatwa baada ya kupatikana kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, ambao unatumika kama kongamano la kuwashawishi vijana wa Kenya kujiunga na ISIS.

Kulingana na hati zilizowasilishwa mahakamani, washawishi sasa wanatumia jukwaa la mitandao ya kijamii kuwasajili vijana kwa makundi ya kigaidi. Bw Hamza na Bw Rashid walipatikana kuwa wanachama wa kikundi cha Telegram kiitwacho Khalifa Tul Umah chenye uanachama Somalia, Tanzania, Congo, Msumbiji na Kenya.

‘Kulingana na ripoti za kijasusi, kundi hilo la Khalifa Tul Umah kwa kiasi kikubwa huchapisha nakala za itikadi kali na nakala zingine zinazothibitisha itikadi kali na ushawishi kuingia kwenye vikundi hivyo,’ Bw Bryzon Wafula wa ATPU alisema.

Bw Hamza na Bw Rashid jana walifikishwa mbele ya Mahakama ya Mombasa, ambapo Hakimu Mkuu Mkazi Vincent Adet aliruhusu ATPU kuwazuilia kwa wiki mbili. Ripoti za kijasusi zilifichua kuwa, Rashid aliondoka Dar es Salam mnamo Novemba 5, akafika Kenya siku hiyo hiyo, na kukutana na Bw Hamza nyumbani kwake Msambweni, kaunti ya Kwale.

Kulingana na ratiba yao, Rashid alitakiwa kusafiri hadi Kenya, kuungana na rafiki yake huko Kwale kabla ya wawili hao kufunga safari ya kwenda Somalia. Wawili hao, hata hivyo, walikamatwa walipokuwa wakielekea Somalia kwa madai ya kujiunga na wapiganaji wa Al-Shabaab.

Stakabadhi walizopatikana nazo kama vitambulisho na vitu vingine vimepelekwa Ofisi ya Taifa ya Usajili na Ubalozi wa Tanzania kwa ajili ya kuthibitishwa. Simu za washukiwa pia zimepelekwa katika Makao Makuu ya ATPU kwa uchunguzi zaidi.

You can share this post!

Wasichana matineja katika hatari – ripoti

Uchovu walemaza kampeni za OKA

T L