Habari Mseto

DCI wafuata iwapo mtoto alitolewa kafara

July 22nd, 2020 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAPELELEZI wanaochunguza mauaji ya kikatili ya msichana wa miaka tisa katika Kaunti ya Murang’a, sasa wanafuatilia uwezekano kwamba huenda alitolewa kafara ya kishetani.

Purity Njeri, ambaye alikuwa mwanafunzi wa gredi ya tatu katika shule ya msingi ya Ihiga-ini, alipatikana ameuawa na mwili wake kupakiwa katika gunia na kuzikwa katika kaburi ndogo shambani mwa familia ya mshukiwa wa miaka 15.

Ripoti ya upasuaji wa mwili ilifichua aliuawa kwa kunyongwa kwa kutumia mikono.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai eneo hilo Bi Juliana Muthini, maafisa wake wanaamini kuwa wako na mshukiwa mkuu katika mauaji hayo lakini uchunguzi zaidi unahitajika kubaini masuala kadhaa ambayo hado hayajang’amuliwa.

Bi Muthini alisema uchunguzi umeonyesha kuwa mshukiwa alikuwa mfuasi wa makanisa kadhaa ambayo imani yake ni ya kutiliwa shaka.

Alisema kabla ya masharti ya janga la Covid-19 kupiga breki waumini makanisani, alikuwa akisafiri akiandamana na wanawake kadhaa hadi nje ya kaunti kuhudhuria ibada.

“Kuna tetesi kuwa huenda kijana huyu alikuwa ametekwa fikra na imani potovu ya utoaji kafara, na uchunguzi wetu unataka kubaini kama alikuwa na ushirika ambao huenda ulimpa kibarua cha kuua msichana huyo,” akasema.

Aliongeza kuwa wanachunguza uwezekano kuwa kijana huyo, ambaye kwa sasa mahakama imetoa idhini ya azuiliwe na wapelelezi hadi Agosti 5 ili asaidie katika uchunguzi, alikuwa na nia ya kumbaka msichana huyo na baada ya kukataa akamuua.

Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua alitembelea familia ya mwendazake na akalalamika kuwa eneo hilo limejaa utumizi wa mihadarati na ulevi miongoni mwa vijana.