Michezo

De Bruyne acheka na nyavu za mapenzi kwa bao kabambe

July 30th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mahiri wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne kwa sasa anatarajia kuwa baba wa watoto wawili na hivyo kuifanya familia yake kuwa ya watu wanne.

Hii ni baada ya mkewe Michele Lacroix kujipata katika ulazima wa kuanza kuhudhuria kliniki kutokana na bao alilofungwa na sogora huyo.

Kufikia sasa, De Bruyne anajivunia mtoto Mason Milian katika uhusiano wake wa kimapenzi na Michele.

Akishindwa kabisa kuyaficha matarajio yake wiki jana, Michele alipakia kwenye mtandao wake wa Instagram picha zake za ujauzito na kuambatanisha maandishi: “Punde tutakuwa familia ya wanne”.

Isitoshe, kichuna huyo alifichua kwamba De Bruyne alimfunga bao hilo litakalohesabiwa mnamo Februari 2019 punde baada ya kipenga cha kuashirikia mwisho wa msimu wa 2017-18 kupulizwa rasmi mnamo Mei 2018.

Michele alimzalia De Bruyne mtoto wao wa kwanza mnamo 2016, miezi mitano baada ya nyota huyo kuagana rasmi na VfL Wolfsburg ya Ujerumani na kutua uwanjani Etihad kuvalia jezi za Man-City.

De Bruyne alimvisha demu wake pete ya uchumba mnamo Desemba 2016 katika mkahawa wa Eiffel Tower jijini Paris, Ufaransa kabla ya kufunga naye pingu za maisha nchini Italia mwishoni mwa Juni 2017.