Michezo

De Bruyne fundi wa soka aliye na hela mfano wa majani ya mkuyu!

May 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KEVIN De Bruyne, 27, ni kiungo mvamizi wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji. Uwezo wake wa kudhibiti mpira kwa miguu yote miwili na kutamba katika nafasi yoyote katika safu ya ushambuliaji ni kiini cha makocha katika ngazi za klabu na timu ya taifa kumwajibisha nyuma ya fowadi mkuu.

Sogora huyo wa zamani wa Chelsea alitokea kambini mwa VfL Wolfsburg nchini Ujerumani mnano 2015 na kutua uwanjani Etihad kuvalia jezi za Man-City katika uhamisho wa mkataba wa miaka sita uliorasimishwa kwa kima cha Sh8.6 bilioni.

Kiasi hicho cha pesa ni cha pili kwa wingi kuwahi kutolewana klabu yoyote ya Uingereza baada ya Sh9 bilioni na Sh14 bilioni zilizotumiwa na Manchester United kujinasia huduma za Angel Di Maria kutoka Real Madrid mnamo 2015 na Mfaransa Paul Pogba kutoka Juventus mnamo 2016.

ASILI: De Bruyne aliishi kwa pamoja na mama yake, Anne kwa zaidi ya miaka 10 nchini Ivory Coast baada mama mzazi kutemana na mumewe, Herwig aliyewahi kuishi pia nchini Burundi. Kwa pamoja na mkubwa wake Stefanie, De Bruyne alilelewa jijini Drongen katika Manispaa ya Ghent, Ubelgiji kuanzia 1991.

UKWASI: Thamani ya mali ya De Bruyne inakadiriwa kufikia Sh3.8 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh12 milioni aliokuwa akipokezwa kwa juma na Wolfsburg kabla ya Man-City kuzinyakua huduma zake kwa ahadi ya Sh35 milioni kila wiki.

Kwa sasa, De Bruyne hutia mfukoni ujira wa hadi Sh49 milioni kwa wiki, malipo ambayo yanamfanya kuwa ? mchezaji ghali zaidi anayedumishwa kimshahara ugani Etihad kabla ya Sergio Aguero, David Silva na Raheem Sterling.

Mbali na mshahara huo mnono, De Bruyne pia hujirinia fedha za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi au kusajili sare akila anapovalia jezi za Man-City au kikosi cha Ubelgiji. Anamiliki kampuni ya kutengeneza nguo aliyoianzisha kwa ubia na shirika la Cult Eleven mnamo 2012.

Japo utajiri wake haujatosha kuutikisa ulimwengu wa masogora ambao kwa sasa wanaoogelea katika bahari ya fedha, De Bruyne ni mwingi wa hisani na mwenye moyo wa kutoa. Asilimia 30 ya mapato yanayovunwa na kampuni yake ya kutengeneza nguo hutolewa kama ruzuku kwa timu ya Olimpiki ya Walemavu nchini Ubelgiji kila mwaka.

MAPENZI NA FAMILIA: De Bruyne alimtema mchumba wake wa muda mrefu, Caroline Lijnen mnamo 2013 baada ya kipusa huyo kusaliti penzi lake alipomrhusu ‘nyani’ nambari moja wa Real Madrid, Thibaut Courtois kulidokoa tunda lake.

Lililomkoroga nyongo zaidi De Bruyne ni kwamba yeye na Courtois walikuwa marafiki wakubwa wakati kipa huyo wa zamani wa Chelsea alipoanza kumtambalia mrembo wake.

MAGARI: Ingawa De Bruyne anamiliki magari mengi ya haiba kubwa, mawili anayoyapenda zaidi ni yale aina ya Ferrari 458 na 918 Spyder ambayo kwa pamoja, yalimgharimu kima cha Sh78 milioni.