Michezo

De Bruyne mwingi wa mizungu, ana hela kama majani ya mkuyu

January 28th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KEVIN De Bruyne, 27, ni kiungo mvamizi wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji. Nyota huyo ni miongoni mwa wanasoka ambao wanapigiwa upatu kuivunia klabu ya Man-City mataji kadhaa nchini Uingereza pamoja na kuipigisha hatua kubwa katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Uwezo wake wa kudhibiti mpira kwa miguu yote miwili na kutamba katika nafasi yoyote ni kiini cha makocha kumwajibisha nyuma ya mvamizi mkuu. Sogora huyo wa zamani wa Chelsea alitokea VfL Wolfsburg mnano 2015 na kutua uwanjani Etihad kwa Sh8.6 bilioni, uhamisho uliorasimishwa kwa kandarasi ya miaka sita.

Kiasi hicho cha pesa ni cha pili kwa wingi kuwahi kutolewana klabu ya Uingereza baada ya Sh9 bilioni na Sh14 bilioni zilizotumiwa na Manchester United kujinasia huduma za Angel Di Maria kutoka Real Madrid mnamo 2015 na Mfaransa Paul Pogba kutoka Juventus mnamo 2016.

ASILI: Japo alizaliwa Burundi, De Bruyne aliishi kwa pamoja na mama yake, Anne kwa zaidi ya miaka 10 nchini Ivory Coast baada mama kutemana na mumewe, Herwig. Kwa pamoja na mkubwa wake Stefanie, De Bruyne alilelewa jijini Drongen katika Manispaa ya Ghent, Ubelgiji kuanzia 1991.

UTAJIRI: Thamani ya mali ya De Bruyne inakadiriwa kufikiaSh3.6 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh11 milioni aliokuwa akipokezwa kwa juma na Wolfsburg kabla ya Manchester City kuzinyakua huduma zake kwa ahadi ya Sh35 milioni kila wiki. Kwa sasa, De Bruyne hutia mfukoni Sh49 milioni kwa wiki, malipo ambayo yanamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi anayedumishwa kimshahara ugani Etihad kabla ya Sergio Aguero, David Silva na Raheem Sterling.

Mbali na mshahara huo, De Bruyne hujirinia fedha za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi. Pia anamiliki kampuni ya kutengeneza nguo aliyoianzisha kwa ubia na shirika la Cult Eleven mnamo 2012.

Japo utajiri wake haujatosha kuutikisa ulimwengu wa masogora wanaoogelea katika bahari ya fedha, De Bruyne ni mwingi wa hisani na mwenye moyo wa kutoa. Asilimia 30 ya mapato yanayovunwa na kampuni yake ya nguo kila mwaka hutolewa kama ruzuku kwa timu ya Olimpiki ya Walemavu nchini Ubelgiji.

MAPENZI NA FAMILIA: De Bruyne alimtema mchumba wake wa muda mrefu, Caroline Lijnen mnamo 2013 baada ya kipusa huyo kusaliti penzi lake alipomrhusu ‘nyani’ nambari moja wa Real Madrid, Thibaut Courtois kulidokoa tunda lake. Lililomkoroga nyongo zaidi De Bruyne ni kwamba yeye na Courtois walikuwa marafiki wakubwa.

na wakihudumu pamoja ugani Stamford Bridge walikokuwa wakivalia jezi za Chelsea.

Hata hivyo, ilimchukua De Bruyne miezi mitatu pekee kujinasia mrembo mwingine, Michele Lacroix aliyemzalia mtoto wa kiume mapema mwaka huu.

Alimvisha Michele pete ya uchumba mnamo Desemba 2016 katika mkahawa wa Eiffel Tower jijini Paris, Ufaransa kabla ya kufunga naye pingu za maisha nchini Italia mwishoni mwa Juni 2017. Michele kwa sasa anatazamia kumzalia De Bruyne mtoto wa pili kufikia Aprili 2019.

MAGARI: Mbali na kumiliki Peugeot RCZ yenye thamani ya Sh6 milioni na Audi A8 iliyomgharimu Sh8 milioni, De Bruynepia ana Mercedes Benz SV12 ya Sh22 milioni.

MAJENGO: Anamiliki kasri la Sh720 milioni jijini Hannover, takriban kilomita 70 kutoka Wolfsburg, Ujerumani. Moja kati ya majengo mawili ya kifahari aliyonayo jijini Brussels, Ubelgiji ni lile la Sh400milioni alilomjengea mama yake mnamo 2013.