Michezo

De Gea arefusha mkataba wake Manchester United

September 18th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KIPA chaguo la kwanza kambini mwa Manchester United, David de Gea amesaini mkataba mpya kuendelea kuwachezea waajiri wake hao hadi mwaka wa 2023.

Kufikia sasa, kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 ameichezea klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mechi 367 tangu asajiliwe na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson mnamo 2011 akitokea Atletico Madrid kwa kitita cha Sh2.4 bilioni.

“Sasa nimeiweka wazi hali yangu ya baadaye na ninachotaka kwa sasa ni kuisaidia klabu hii kushinda mataji huku nikiwa na matumaini makubwa ya ndoto hiyo kutimia,” alisema mlinda-lango huyo raia wa Uhispania.

“Nashukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na klabu hii maarufu kwa kipindi cha miaka minane iliyopita.”

De Gea, ameichezea timu ya taifa ya Uhispania mara 40, mbali na kuisaidia Man-United kutwaa ubingwa wa taji la EPL katika msimu wa 2012-13, Kombe la FA Cup miaka mitatu baadaye pamoja na League Cup na Europa League msimu wa 2016-17.

Mhispania huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Real Madrid mara kadhaa, na alitarajiwa kujiunga na vigogo hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mapema mwaka 2019, lakini hakufanikiwa.

Awali, alikaribia pia kujiunga na klabu hiyo iliyokuwa tayari kutoa Sh3.7 bilioni mnamo Septemba 2015, lakini dili hiyo iliambulia patupu.

Kusuasua kwa Man-United kurefusha kandarasi ya kuhudumu kwake uwanjani Old Trafford ni jambo lilowafanya Juventus ya Italia na Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa kuanza kuyahemea maarifa yake mwanzoni mwa msimu huu.

Wingi wa tetesi za kubanduka kwa De Gea uliwachochea Man-United kuanza kuziwania huduma za Jan Oblak wa Atletico Madrid kuwa kizibo cha kipa huyo matata.

Tangu kuondoka kwa Alexis Sanchez aliyejiunga na Inter Milan ya kocha Antonio Conte kwa mkopo wa msimu mmoja, Man-United wamekuwa wakimsihi De Gea kutia saini mkataba mpya kwa ujira wa hadi Sh46 milioni kwa wiki.

Kiini cha Conte kuyawania maarifa ya De Gea ni katika jitihada za kulijaza pengo la ‘nyani’ wa zamani wa Arsenal, Wojciech Szczesny ambaye amekuwa akisuasua langoni katika siku za hivi karibuni.