Michezo

De Gea asema Manchester United ya sasa sio kama ya zamani

October 8th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KIPA David de Gea wa Manchester United amefichua uwezekano wa kubanduka kambini mwa kikosi hicho iwapo hakitajinyanyua na kuanza kusajili matokeo ya kuridhisha katika kampeni za msimu huu.

Mlinda-lango huyu mzawa wa Uhispania amekiri kwamba matokeo duni ambayo kwa sasa yanaandikishwa na waajiri wake katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hayakubaliki na huu ndio msimu wake mgumu zaidi uwanjani Old Trafford tangu ajiunge na Man-United.

De Gea alisajiliwa na Man-United mnamo 2011 baada ya kuagana rasmi na miamba wa soka ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid.

Mnamo Jumapili, Man-United almaarufu ‘The Red Devils’ walIpokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Newcastle United uwanjani St James’ Park na hivyo kuendeleza matokeo mabovu zaidi katika historia yao 1989.

Kichapo kutoka kwa Newcastle wikendi iliyopita kiliwasaza Man-United katika nafasi ya 12 jedwalini kwa alama tisa sawa na Brighton na limbukeni Sheffield United.

Ni alama mbili pekee ndizo zinazowatenganisha Man-United na vikosi vilivyopo katika mduara wa kuteremshwa daraja.

“Masihara haya ya Man-United hayakubaliki. Haiwezekani kabisa kwa kikosi kuendelea kucheza kama inavyozidi kushuhudiwa msimu huu. Timu haikujitengenezea nafasi zozote za kutatiza mabeki wa Newcastle,” akatanguliza De Gea.

Aidha, anasema kikosi kimekosa makali yanayohitajika.

“Tuna mengi ya kufanya ili kujiimarisha na kuwekea dira kampeni zetu za baadaye. Ingawa tuna visa vichache vya majeraha, hatuna sababu yoyote ya kutofanya vizuri ligini,” akaongeza De Gea huku akiwahimiza wenzake wajitahidi maradufu mazoezini na kurejelea ubora utakaoanza kuwavunia matokeo ya kuridhisha.

Kiungo Matty Longstaff, 19, aliwafungia Newcastle bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo uliowashuhudia wakitia kapuni alama tatu muhimu zilizowapaisha hadi nafasi ya 16 jedwalini sawa na Aston Villa.

Man-United kwa sasa hawajasajili ushindi wowote kutokana na mechi nane zilizopita ugenini. Ushindi wao wa mwisho ni kivumbi kilichowashuhudia wakiwachapa Crystal Palace 3-1 ugani Selhurst Park mnamo Februari 27, 2019.

Matokeo ya Man-United ndiyo mabovu zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi hiki cha kocha Ole Gunnar Solskjaer katika historia yao tangu Septemba 1989.

Baada ya kumenyana na Newcastle, Man-United kwa sasa wanajiandaa kuwaalika viongozi wa EPL, Liverpool uwanjani Old Trafford mnamo Oktoba 20.