Deby azikwa huku jeshi la nchi likigawanyika kuwili

Deby azikwa huku jeshi la nchi likigawanyika kuwili

Na AFP

N’DJAMENA, CHAD

RAIS wa Chad aliyefariki baada ya kujeruhiwa vitani, Idriss Deby Itno, alizikwa Ijumaa katika mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi wa mataifa tofauti akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Viongozi hao walikaidi onyo la waasi waliomuua Deby na kusafiri hadi jiji kuu la Chad, N’Djamena, kuhudhuria mazishi yake huku viongozi wa upinzani wakipinga hatua ya jeshi kumtwika mwanawe, Jenerali Mahamat Deby Itno uongozi wa nchi hiyo.

Zaidi ya viongozi wa nchi 12 walihudhuria mazishi ya kitaifa katika bustani ya La Place de la Nation jijini N’Djamena kabla ya mwili wa Deby kusafirishwa kwa ndege hadi kijiji cha Amdjarass, Berdoba, karibu na mpaka wa Chad na Sudan alikozikwa.

Chad, ni nchi inayoheshimiwa na muhimu kwa kupiga vita ugaidi katika eneo la Sahel, ambako makundi mengi ya kigaidi yamepiga kambi.

Kikosi cha wanajeshi 5,100 wa Ufaransa, maarufu kama Barkhane, kinachopigana na magaidi kina makao yake makuu N’Djamena.

Chad ilitumbukia katika hali isiyotabirika baada ya kifo cha Deby, siku moja baada ya kushinda muhula wa sita kuongoza nchi hiyo baada ya kutawala kwa miaka 30.

Jeshi lilisema Deby alifariki Jumatatu baada ya kujeruhiwa akiongoza wanajeshi kupigana na waasi waliovamia nchi hiyo kutoka Libya.

Waasi wa The Front for Change and Concord in Chad (FACT) wameapa kuendeleza mapigano baada ya mazishi ya Deby huku msemaji wao Kingabe Ogouzeimi de Tapol akiambia shirika la habari la AFP kwamba, wanaelekea N’Djamena.

Mnamo Jumatatu, siku ambayo kifo cha Deby kilitangazwa, jeshi lilidai ushindi mkubwa dhidi ya waasi hao likisema limeua zaidi ya waasi 300 wa FACT na kuwateka nyara wengine 150. Walisema kwamba wanajeshi watano waliuawa.

Wakati huo huo, washirika wa hayati Deby walichukua hatua za haraka kuhakikisha mamlaka hayawaponyoki kwa kumtawaza mwanawe Mahamat, 37, anayefahamika kama Kaka, kuwa rais na mkuu wa baraza la mpito la kijeshi huku wakivunja bunge na serikali.

Upinzani umetaja hatua hiyo itakayodumu kwa miezi 18 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika kama mapinduzi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema jeshi lilikuwa na haki kumtawaza Deby kwa kuwa spika wa bunge alikataa kutwaa majukumu ya rais.

“Kwa kawaida, inafaa kuwa Spika (Haroun) Kabadi, lakini alikataa kwa sababu za kiusalama ambazo zinahitajika kuhakikisha uthabiti katika nchi hii,” Le Drian aliambia runinga ya France 2.

You can share this post!

Brenda Ochieng anavyotesa katika tasnia ya uigizaji

IRENE MUKUSYA: Ninalenga kupaa anga za kimataifa kwa...