‘Deep State’ ilivyozima mashujaa

‘Deep State’ ilivyozima mashujaa

Na TAIFA RIPOTA

VIONGOZI wa kisiasa na mabwanyenye wamelaumiwa kwa kuwa kikwazo kikuu cha Wakenya kufurahia matunda ya mashujaa waliopigania uhuru.

Kulingana na ripoti ya majuzi kuhusu hali ya demokrasia nchini, serikali ambazo zimeongoza Kenya tangu 1963 zimekuwa zikiendeleza utawala wa kunyanyasa raia, ambao zilirithi kutoka kwa wakoloni Waingereza.

“Utawala wa kikoloni ulikuwa wa kunyanyasa Waafrika. Baada ya uhuru, viongozi waliochukua madaraka waliendeleza utawala huo wa kidikteta. Uhuru haukubadilisha chochote ila tu kupokeza unyanyasaji kwa Waafrika,” yasema ripoti hiyo ya “Democracy Capture in Kenya”.

Kulingana na ripoti hiyo, baada ya Kenya kupata uhuru, mashujaa wa Mau Mau waliokuwa mstari wa mbele kupigania uhuru waliwekwa kando, na badala yake madaraka yakatwaliwa na waliokuwa wakiunga mkono ukoloni hasa machifu na watoto wao.

“Kwa kushirikiana na wakoloni, machifu na washirika wao walituzwa kwa mashamba, nyadhifa kuu serikalini, kibali cha kukuza mazao kama kahawa na chai na manufaa mengine ya kiuchumi. Hali hii iliweka msingi wa Kenya kuwa mikononi mwa kundi ndogo la viongozi wakuu na mabwanyenye,” inaeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inamlaumu rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta kwa kile inasema ni kukoroga mpango wa kuweka uchumi mikononi mwa Waafrika, kwani aliwapendelea waliokuwa washirika wa wakoloni na marafiki wake wa karibu.

Uthibiti huu wa uchumi na kundi ndogo la mabwanyenye uliimarishwa miaka ya sabini wakati serikali ilipokubali wafanyikazi wake kumiliki biashara.

“Maafisa wa umma walitumia fursa hiyo kupora mali ya serikali, hali ambayo iliweka msingi wa ufisadi nchini na utekaji wa nchi na kundi ndogo maarufu kama ‘Deep State’.

“Kutokana na manufaa wanayopata, maafisa hawa wanakuwa na usemi mkubwa kuhusu nani anachukua uongozi wa nchi katika juhudi za kulinda maslahi yao.

“Hatima yake imekuwa ni kutekwa kwa demokrasia ya Kenya, ambapo kundi hilo linahusika katika kufadhili kampeni na kukoroga taasisi za kusimamia uchaguzi katika juhudi za kuhakikisha “mtu wao” ndiye anashinda.

“Watu hao wanashirikiana na wenzao kutoka sekta ya kibinafsi na vyombo vya usalama, ambapo wamebuni ‘Deep State’ ambayo ndiyo yenye usemi wa mwisho kuhusu nani anachaguliwa na pia nchi inavyotawaliwa.

“Katika chaguzi za 2013 na 2017, wafanyibiashara wakubwa na maafisa wakuu serikalini walifadhili kampeni za uchaguzi. Wanafanya hivyo kulinda maslahi yao na kuendelea kuwa na usemi kuhusu anayekuwa rais.”

Ripoti hiyo inasema kuwa lengo kuu la mabwanyenye na washirika wao serikalini kuteka demokrasia nchini ni kwa ajili ya kuendelea kujitajirisha zaidi kwa raslimali za kitaifa.

“Wakati wa ukoloni dhamira ilikuwa kuhamisha mali ya umma hadi ng’ambo. Siku hizi lengo ni kutajirisha wachache. Kwao usemi wa ni nani atakuwa rais ni muhimu sana kwani analinda maslahi yao.

“Ukabila nao unatumika kushawishi watu waunge mkono ‘mtu wao’ kuwa rais kwa imani kuwa akiwa madarakani watasaidika kiuchumi. Lakini hili huwa halifanyiki. Matokeo ya kila uchaguzi yanakuwa ni njama tu ya kuwafaa wachache wa tabaka la juu.”

Kulingana na ripoti hiyo, kundi hili la “Deep State” ndilo limekuwa kikwazo kwa utekelezaji kamilifu wa Katiba ya 2010 kwa hofu kuwa itavuruga ushawishi wao wa kisiasa na kiuchumi.

Inasema kuwa kura zinazopigwa na Wakenya kila baada ya miaka mitano huwa tayari zimekorogwa.

“Tangu 1992, chaguzi zimekuwa tu ada kwa “Deep State” kuidhinisha wanayemtaka kuwa rais. Hii imefanya serikali kuwa haiwajibiki kwa wananchi bali kwa waliyoiweka mamlakani.

“Baada ya kuthibiti mfumo wa uchaguzi, ‘Deep State’ hugeukia vyombo vya habari na mashirika ya kijamii. Vyombo vya habari huzimwa kwa vitisho vya kupokonywa matangazo na shinikizo kutoka kwa maafisa wa serikali. Pia wanaendeleza propaganda katika mitandao ya kijamii. Mbinu nyingine ni kugawanya wananchi kikabila kupitia kubuniwa kwa vyama vya kikabila,” inasema ripoti.

Ripoti hiyo pia inashutumu “Deep State” kwa kuingilia uhuru wa mahakama kupitia uthibiti wa Tume ya Mahakama (JSC), kupuuza maamuzi ya JSC, kuipunguzia mgao wa bajeti na kuingilia uhuru wa majaji.

You can share this post!

Salah avunja rekodi ya ufungaji wa mabao ya UEFA kambini...

GWIJI WA WIKI: Georginah Nyatichi

T L