Makala

Del Monte yasajili G4S kulinda mananasi kwa mazingira ya kuheshimu haki za binadamu

March 6th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

HUKU ikiandamwa na shutuma kali kwamba walinzi wake huwaua majirani wanaoshukiwa kuiba mananasi yake, kampuni ya Del Monte sasa imewafuta kazi walinzi 270 na kusajili kampuni ya G4S kudumisha usalama katika shamba lake la zaidi ya ekari 25,000.

Sasa kampuni ya G4S ndio itakuwa ikitoa huduma za ulinzi katika shamba hilo kupitia walinzi 270 ambao taarifa ya Machi 5, 2024, ya Del Monte ilisema kwamba tayari wamesajiliwa.

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Uhusiano Mwema wa Del Monte Muthoni Wachira, ilisema kwamba lengo kuu la walinzi hao wapya ni kusaidia kampuni hiyo kukabiliana na magenge ya wizi wa mananasi kwa njia isiyokinzana na haki za binadamu.

Alisema kwamba walinzi hao wamepewa uhamasisho wa kina kuhusu namna ya kuepuka utumizi wa mabavu kupindukia, kuheshimu haki ya uhai na kujadiliana na wenyeji badala ya kuingia moja kwa moja ndani ya vurugu za kivita.

Katika siku za hivi karibuni, majirani wa kampuni hiyo ambayo shamba lake husambaa katika kaunti za Kiambu na Murang’a, wamekuwa wakilalama kwamba vijana ambao hujitafutia riziki kupitia wizi wa mananasi wamekuwa wakiuawa kikatili na walinzi.

Aidha, Seneta wa Murang’a Joe Nyutu amekuwa katika mstari wa mbele kuteta kwamba mauaji hayo yamekuwa yakifanyika kisiri na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huenda zaidi ya watu 500 wameuawa na miili yao kutupwa katika mito na mabwawa yaliyo karibu.

Ni hali ambayo imetatiza usimamizi wa shamba hilo kwa kiwango kikuu kiasi kwamba hata baadhi ya masoko ya ng’ambo yamekuwa yakisusia bidhaa za kilimo kutoka kampuni hiyo ya Del Monte kwa msingi wa kuhusishwa na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Serikali ya Kenya nayo imejipata ikisukumwa si haba ikabiliane na madai hayo kwamba kampuni ya Del Monte imekuwa ikichangia maafa kutokea, huku pia wanawake wakibakwa na kujeruhiwa kwa msingi wa kisingizio cha utekelezaji wa doria dhidi ya wezi wa mananasi.

Kwa sasa, watu 12 wamewasilisha kesi mahakamani dhidi ya maafisa serikalini na pia kampuni ya Del Monte, wakisaka amri za kusitishwa kwa mauaji, uvamizi na matukio mengine yoyote ya ukiukaji wa haki za kibinadamu dhidi ya majirani wa kampuni hiyo.

Kesi hiyo ambayo ni ya Desemba 30, 2023, katika Mahakama Kuu ya Thika na ambayo imenakiliwa kama HCCHRPET/E002/2023 iko katika awamu ya kusikilizwa.

Wale ambao wameshtakiwa katika kesi hiyo kando na Del Monte ni Waziri wa usalama wa ndani Bw Kithure Kindiki, Inspekta Mkuu wa Polisi Bw Japhet Koome Mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) Bw Mohammed Amin, Mwenyekiti wa tume huru ya kumulika utenda kazi wa polisi (Ipoa) Bi Anne Makori, Mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Bw Renson Ingonga na Mwanasheria Mkuu, Bw Justin Muturi.

Taifa Leo imedokezewa kwamba Marekani imekuwa ikiweka presha kwa Kenya isaidie Del Monte kudhibiti wizi wa mananasi ndipo uvamizi wa magenge upungue hivyo basi kuondoa makabiliano ya kuzua mauti.

Kampuni hiyo pia imekuwa ikiteta kwamba walinzi wake huvamiwa na kuuawa huku wengine wakisababishiwa majeraha mabaya katika makabiliano hayo dhidi ya wezi wa mananasi.

“Tuliitwa katika mkutano wa kuangazia usalama mnamo Januari 14, 2024, na tukaambiwa kwamba Del Monte ni kampuni muhimu katika uhusiano kati ya Marekani na Kenya. Tuliambiwa ni lazima tungesaidia kampuni hiyo kurejea katika soko lake la kimataifa baada ya kupigwa marufuku na baadhi ya wateja kutokana na rekodi mbovu ya haki za kibinadamu. Tuliambiwa mauaji yaliyokuwa yakiripotiwa yalikuwa yakitokana na uzembe wetu wa kupigana na magenge ya wizi,” akasema mmoja wa maafisa wakuu wa usalama katika Kaunti ya Murang’a.

Kampuni hiyo ya Del Monte imeajiri moja kwa moja zaidi ya Wakenya 6,500 na wengine zaidi ya 28,000 wakijipa riziki kupitia uhusiano nayo.

Bajeti ya mshahara ya kampuni hiyo ni zaidi ya Sh2.7 bilioni kwa mwaka huku ikinunua bidhaa za zaidi ya Sh4 bilioni kwa mwaka na kulipa zaidi ya Sh1.4 bilioni kama ushuru kila mwaka.

Mdokezi huyo alikiri kwamba serikali ilikuwa na msimamo kwamba kampuni hiyo ni kiungo thabiti cha kuunda nafasi za kazi na pia kuchangia upanuzi wa uchumi wa nchi hivyo basi kukubaliana na Marekani kwamba kulikuwa na haja ya kusaidiwa ili iepuke presha za kimataifa, za majirani na za wanasiasa.

Tayari, Kamanda wa polisi wa Murang’a Kainga Mathiu ameanzisha mpango kabambe kukabiliana na magenge ya wizi yanayolenga mali ya Del Monte chini ya Operesheni Linda Mananasi.

Alisema kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, imekadiriwa kwamba kampuni hiyo hupoteza zaidi ya Sh7.5 milioni kwa mwezi kupitia wizi huo.

[email protected]