Michezo

Dele Alli aambiwa ayoyomee PSG

September 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamefichua azma ya kumsajili fowadi raia wa Uingereza, Dele Alli, 24, kutoka Tottenham Hotspur.

Wanafainali hao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wanafuatalia hali ya kiungo huyo mvamizi ambaye nafasi yake inatazamiwa kutwaliwa na Gareth Bale aliyerejea Spurs kutoka Real Madrid.

Dalili za kuashiria kutokuwepo kwa Alli katika mipango ya baadaye ya kocha Jose Mourinho zilijidhihirisha wakati wa mechi iliyowakutanisha Spurs na Lokomotiv Plovdiv ya Bulgaria kwenye mchujo wa Europa League mnamo Septemba 17.

Sogora huyo aliondolewa ugani mwishoni mwa kipindi cha pili dhidi ya Plovdiv na akaachwa nje kabisa katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililoshuhudia Spurs wakiwapepeta Southampton 5-2 mnamo Septemba 20 ugani St Mary’s.

Bale alitua Spurs kwa mkopo mnamo Septemba 19 na anatazamiwa kuunga kikosi cha kwanza cha Mourinho dhidi ya West Ham United mnamo Oktoba 17 baada ya kupona jeraha alilopata akichezea Wales mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa kuwa muhula wa uhamisho wa wachezaji unafungwa rasmi Oktoba 5, 2020, ina maana kwamba Alli ana chini ya majuma mawili kuamua mustakabali wake: ama kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za PSG au kusalia Spurs kusugua benchi.

Katika mahojiano yake na wanahabari mwishoni mwa mechi dhidi ya Southampton, Mourinho alisisitiza kwamba kiini cha kuachwa kwa Alli nje ya gozi hilo ni wingi wa wanasoka walio na uwezo wa kucheza katika nafasi yake kwa sasa.

Wanasoka hao waliokuwa wkairejelewa na Mourinho ni Bale, Son Heung-min, Lucas Moura, Harry Kane, Moussa Sissoko, Erik Lamela na Steven Bergwijn.

Hadi kufikia sasa, Alli amechezeshwa kwa dakika 45 pekee msimu huu – dhidi ya Everton waliowalaza 1-0 nyumbani.

Baada ya kujiunga na Tottenham kutoka MK Dons mnamo 2015, Alli aliimarika na kuwa miongoni mwa wanasoka tegemeo chini ya kocha Mauricio Pochettino.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO