Delmonte: Wakazi wa Gatuanyaga wakerwa kwa kutohusishwa kikamilifu kwenye suala la umiliki ardhi

Delmonte: Wakazi wa Gatuanyaga wakerwa kwa kutohusishwa kikamilifu kwenye suala la umiliki ardhi

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatuanyaga, Thika Mashariki, wamelalamika kutokana na kile wamedai ni unyakuzi wa shamba la Delmonte.

Kampuni ya Delmonte hivi majuzi ilipeana ekari 672 za ardhi kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu kwa minajili ya kupanua kaunti hiyo.

Hata hivyo wakazi hao wanahofia kuna njama za watu fulani kuvamia shamba hilo kwa manufaa yao wenyewe.

Wakazi hao wanahofia kuwa tayari kuna watu wenye ushawishi ambao wanajitakia makuu kwa kutaka kumiliki maeneo ya ardhi hiyo.

Mwenyekiti wa Gatuanyaga Residents Association, Bw David Chege, alisema hakuna wakati wowote wananchi wamejulishwa kuhusu ardhi hiyo ambayo ndiko yaliko makazi yao.

“Sisi kama wakazi wa hapa Gatuanyaga hatujapata kuarifiwa jinsi ardhi hiyo itakavyogawanywa. Tunastahili kupewa mwongozo jinsi tutanufaika na ardhi hiyo,” alisema Bw Chege.

Mwenyekiti huyo alipendekeza mambo manne muhimu ambayo wangetaka yazingatiwe.

Kwanza wanapendekeza wao kama wakazi wa Gatuanyaga wahusishwe kwa mazungumzo yoyote kuhusu eneo hilo.

Wanataka Gavana wa Kiambu Bw Kimani Wa Matangi kuzungumza nao ili waelewane kuhusu eneo lao.

Walipendekeza wapewe eneo Bunge lao ili wawe na mambo yao wenyewe kimaendeleo.

Walitaka pia serikali kuu kuingilia kati ili kuwaokoa kutoka kwa wanyakuzi wa ardhi yao.

Askofu wa kanisa la Calvary Chosen Centre Bw David Gakuyo aliwashauri wakazi wa Gatuanyaga waungane ili waweze kupata haki yao ipasavyo.

“Nyinyi kama wakazi wa hapa Gatuanyaga msikubali wageni kutoka nje Juja kujigawia ardhi yenu,” alisema Bw Gakuyo

Inadaiwa ya kwamba kaunti ya Kiambu ina mipango kabambe ya  kuendeleza ardhi hiyo waliopokea kutoka kwa kampuni ya Delmonte.

Kaunti ya Kiambu inapanga kujenga majumba za orodha za kuishi, uwanja wa ndege, sehemu za juakali, na mambo  mengine yanayostahili.

Wakazi hao kwa kauli moja wanasema jambo lolote litakalopangwa na kaunti ya Kiambu ni sharti wahusishwe na wakubaliane kikamilifu.

Waliapa kuwa hakuna shamba lao litafanyiwa maendeleo bila wao kuarifiwa na kupewa mwelekeo mwafaka.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Magoha alionyesha umuhimu wa watu kubuni na...

Serikali yapanga kupunguza ada ya NHIF

T L