Demu afumaniwa akiroga wakwe

Demu afumaniwa akiroga wakwe

Na John Mutuku Samuel

Kisa cha kushangaza kilitokea mtaani hapa, baada ya demu aliyezuru wazazi wa mumewe kufumaniwa usiku akirandaranda kote akiwa nusu uchi.

Mdokezi wetu alituarifu kuwa, polo na demu waliwasili mtaani kutoka jijini Nairobi na kulakiwa kwa moyo mkunjufu.

Demu alichukua usukani, akiwa bingwa wa mapishi, akawaandalia watu wote wakala wakajiramba vidole.

‘Mwanangu, una bahati kama mtende kumpata mkazamwana kama huyu. Huyu ndiye nilikuwa nikiomba ujaaliwe,’ mavyaa alisema. Mazungumzo marefu yaliendelea hadi saa tano usiku.

Kila mmoja alikuwa mchovu na mwenye usingizi mwingi. Waliagana alamsiki kisha polo na demu wakaingia chumba chao kulala.

Mnamo saa saba usiku, demu aliamka polepole na kutoka. Hakuwa na vazi la kusitiri uchi wake.

Polo hakusikia wala mavyaa. Hata hivyo bavyaa alisikia mlango ukifunguliwa taratibu.

Naye aliamka na kunyata hadi akaufungua.Demu alipotoka nje, alianza kuzunguka nyumba, akikimbia kama mwanariadha.

Bavyaa alipomuona mke wa mwanawe alishtuka sauti ikampotea.’Jamani, tuliyemsifu kwa upishi kumbe ni mchawi? Hata hana aibu akiroga ugenini siku ya kwanza tu,’ bavyaa alishangaa.

Haukupita muda, bavyaa alipiga mayowe lakini hayakumshtua demu. Watu waliamka na hata majirani walifika.

Demu alikamatwa lakini akaomba asichapwe.Walitokea wanawali wakamfunga leso kisha akawekwa ndani ya chumba maalum kusubiri mapambazuko.

‘Naomba msiniue jamani. Nimetumwa kutekeleza mambo haya na mama yangu mzazi,’ demu alikiri.

Adai kwamba mama yake alimwambia kwamba akiwaroga atakuwa amemiliki boma hilo na hangepatwa na mikosi ya aina yoyote katika ndoa yake. Saa kumi na moja, alitafutiwa nauli, akaamriwa kutokanyaga huko tena.

 

You can share this post!

Italia waponda Jamhuri ya Czech kirafiki na kuvuna ushindi...

Pigo kwa Serikali korti ikiruhusu Miguna kurejea