Dondoo

Demu afurusha mpenzi kwa ulevi

August 4th, 2019 1 min read

NA MIRRIAM MUTUNGA

NAARI, MERU

MWANADADA wa hapa alipongezwa na majirani kwa kumkana mpenzi wake alipomtembelea akiwa mlevi.

Penyenye za mtaani zinasema kwamba jamaa alikuwa amechukua muda bila kumtembelea demu jambo lililomfanya mwanadada kuanza kulalamika na kutishia kumtema iwapo hangetembelea.

Juzi, jamaa alimpigia simu kipusa na kumjulisha kwamba angemtembelea.

Siku ya tukio, demu alijiandaa tayari kumpokea mpenzi wake asijue kilichokuwa kikimsubiri. Inaarifiwa demu hakuamini macho yake alipomuona mpenzi wake akiwa amelewa chopi na kuropokwa cheche za maneno.

“Jamaa aliwasili katika ploti akiwa mlevi. Alikuwa akitembea kwa shida na kuropokwa maneno yasiyo ya heshima,” alisema mdokezi.

Ni katika hali hiyo demu alipopandwa na mori na kuanza kumfokea jamaa.

“Wewe ni nani na unafanya nini hapa? Peleka ulevi wako ulikotoka,” demu alimwambia jamaa alipobisha mlango wa nyumba yake.

Inasemekana jamaa alikataa kuondoka huku akimtaka demu waingie chumbani lakini demu akampuuza.

“Nimekwambia uondoke hapa kwangu mimi sikujui wala sina haja na wewe.Hiki si kilabu,”demu alimwambia jamaa kwa hasira.

Demu aliingia ndani ya nyumba na kumfungia jamaa nje.Inasemekana jamaa alilazimika kuondoka huku akijutia tabia yake. Kulingana na mdokezi, jamaa alimkosea sana mwanadada huyo ambaye anajulikana katika ploti kwa kudumisha heshima ya hali ya juu.

“Ni mwanadada anayeheshimiwa na watu kwa tabia yake nzuri. Hakuna mwanamume mwingine anayeingia katika nyumba yake,” alisema mdokezi.

Hata hivyo haikujulikana iwapo jamaa aliwasiliana na demu baada ya pombe kupungua mwilini. “Demu hakubadilisha tabia hata baada ya kisanga hicho,” alisema mdokezi.